Na mwandishi wetu, Gazetini
NI JUMAPILI ya wiki hii, Januari 4, 2025. Taifa Stars itakapoumana na Morocco katika mchezo wa hatua ya 16 Bora ya fainali za mwaka huu za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Mchezo huo wa kusaka robo fainali utachezwa mjini Rabat katika Uwanja wa Moulay Abdellah Sports Complex.
Wenyeji wa michuano, Morocco, walivuka hatua ya makundi wakiwa na ushindi wa mechi mbili na sare moja.
Katika mchezo wa kwanza, waliifunga Comoro mabao 2-0, kisha ushindi wa mabao 3-0 dhid ya Zambia, kabla ya sare ya bao 1-1 walipokutana na Mali.
Kwa upande wake, Stars iliweka historia ya kuingia kwa mara ya kwanza hatua ya 16 Bora ya mashindano hayo ya Shirikisho la Soka barani Afrika (AFCON 2025).
Chini ya kocha wa kigeni raia wa Argentina, Miguel Gamondi, Stars ilivuka makundi kwa dirisha la ‘best loser’ baada ya sare mbili katika mechi zake tatu.
Katika mchezo wa kwanza, Stars walifungwa mabao 2-1 na Nigeria, kisha kulazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi mbili zilizofuata dhidi ya Uganda na Tunisia.
Hata hivyo, kuelekea mchezo dhidi ya Morocco, Stars haina rekodi nzuri katika mechi ilizokutana na vigogo hao wa soka la Afrika ya Kaskazini.
Katika michezo nane, Morocco imeshinda saba, ukiwamo ushindi wa mabao 3-0 mara ya mwisho timu hizo zilipokutana.
Je, baada ya kumaliza ‘unyonge’ wa kuishia hatua ya makundi katika michuano ya AFCON, Stars itaishangaza Morocco wikiendi hii?


