RABAT, Nigeria
KOCHA wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi, ameweka wazi kuwa vijana wake hawatotanguliza hofu mbele ya Nigeria ‘Super Eagles’.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Desemba 23, 2025, ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa pande zote wa hatua ya makundi msimu huu wa fainali za Mataifa Afrika (AFCON).
Licha ya kukiri kuwa wapinzani wao hao wana ubora mkubwa, Gamondi raia wa Argentina amesema Stats imejiandaa kwa michuano mkubwa, hivyo hakuna cha kuhofia.
Amesisitiza kuwa vijana wake wanapaswa kuelekeza akili yote uwanjani, pia kufuata maelekezo waliyopewa na benchi la ufundi.
“Hupaswi kushambulia sana unapocheza dhidi ya Nigeria. Ukitazama ubora mkubwa walionao wachezaji wao, unapaswa kujitoa kwa asilimia zaidi ya 100 ndani ya uwanja,” amesema.
“Jambo muhimu kwetu ni kubaki kwenye muundo wetu, nidhamu ya kiufundi … Katika mechi kama hii, hupaswi kufanya makosa mengi ndani ya uwanja.”


