Na mwandishi wetu, Gazetini
KAMA kuna alama isiyofutika na itakayobaki kwa miaka mingi katika historia ya soka la Tanzania, basi ni kile alichokifanya Mbwana Samatta.
Mchezaji pekee raia wa nchi hii kuwahi kucheza Ligi Kuu ya England (EPL) aliposajiliwa na Aston Villa mwaka 2020 kwa ada ya Pauni milioni 8.5 akitokea Genk ya Ubelgiji.
Kama hiyo haitoshi, akaweka rekodi nyingine kubwa akiwa Villa. Mchezaji pekee wa Tanzania kufunga bao katika mechi ya fainali ya Kombe la Ligi England (Carabao Cup), ingawa Villa ilifungwa na Manchester City.
Hata baada ya kushindwa kung’ara EPL, bado alama ya Samatta katika soka la Ulaya haikuzima ghafla, na badala yake alisajiliwa na klabu nyingine kubwa barani humo, Fenerbahce.

Kwa sasa, bado alama ya Samatta inaendelea kuitangaza Tanzania akiwa Ligue ya Ufaransa, ambayo pia ni miongoni mwa Ligi Kuu tano bora barani Ulaya.
Ndiyo, Samatta anaitumikia Le Havre na msimu huu ameshapata nafasi ya kushika dimbani katika mechi 11 za Ligi Kuu hiyo.
Hakika ni historia ya pekee na hata kama itatokea kwa Tanzania kupata mchezaji mwingine kucheza EPL na Ligue 1, basi bado Samatta atabaki kuwa ndiye aliyechonga barabara hiyo.
Kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Desemba 21, mwaka huu, Samatta atakwenda Morocco akiwa si tu nahodha, bali pia kiongozi wa safu ya ushambuliaji.
Ikionekana wazi kuwa ni msimu wake wa mwisho kucheza fainali hizo akiwa kwenye kiwango bora alichonacho sasa, ingawa pia anaweza kuwapo mwaka 2027, Samatta ana mtihani mkubwa ulio mbele yake.
Kama nahodha, Stars itasaka ushindi wa kwanza katika historia ya AFCON. Licha ya kushiriki mara tatu (1980, 2019 na 2023), haijawahi kupata ushindi wa mechi ya michuano hiyo.
Katika fainali za mwaka 1980 zilizofanyika Nigeria, Stars ilimaliza mkaini mwa Kundi A ikiwa na pointi moja baada ya kuambulia sare moja kwenye mechi tatu. Mwaka 2019, ikiwa Kundi C haikupata pointi, kama ilivyokuwa mwaka 2023 (Kundi F).
Ni kwa maana hiyo, itakuwa ni heshima kubwa kwake endapo ataiongoza Stars kupata ushindi wa kwanza kwenye fainali hizo au hata kuvuka hatua ya makundi.
Hata hivyo, hata kama yote yatashindikana, bado haiondoshi ukweli kwamba Samatta anabaki kuwa kielelezo cha mafanikio ya wachezaji wa Tanzania. Mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa kizazi cha sasa katika kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.


