DAR ES SALAAM, Tanzania
KATIKA fainali za Mataifa ya Afrika msimu uliopita, 2024, Taifa Stars ilikuwa sehemu ya timu zilizokuwa gumzo kwa kiasi fulani kwenye michuano hiyo.
Stars Ilimfuta kazi kocha wake raia wa Algeria, Adel Amrouche, baada ya mechi moja tu. Uamuzi wa kumfukuza ulitokana na kauli ya kocha huyo, alipoishutumu Morocco kwa madai kuwa imekuwa ‘ikibebwa’ na waamuzi.
Amrouche alienda mbali zaidi na kusema Morocco imekuwa na ushawishi wa kuamua mwamuzi wa kuchezesha mechi fulani. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilimfungia mechi nane, pamoja na kumtoza faini ya Dola 10,000.
Hata hivyo, Amrouche hakuwa kocha pekee aliyepoteza kibarua katika hatua za mwanzo za michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika.
Wengine kwenye orodha hiyo ni Chris Hughton (Ghana), Djamel Belmadi (Algeria), Jalel Kadri (Tunisia) na Tom Saintfiet (Gambia).


