9.8 C
New York

Alidumu siku 80 tu Yanga, sasa shujaa wa Mali akielekea AFCON

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MALI ni moja ya mataifa 24 yatakayokuwa nchini Morocco kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka huu (AFCON 2025) zitakazoanza rasmi Desemba 21.

Katika benchi la ufundi, timu yao ya taifa ‘Eagles’ inajivunia uwepo wa Tom Saintfiet, kocha wa kimataifa wa Ubelgiji, ambaye ana historia ya aina yake hapa Tanzania.

Saintfiet aliajiriwa Yanga mwaka 2012 akiwa kocha wa kwanza raia wa Ubelgiji kukabidhiwa benchi la ufundi katika historia ya klabu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani.

Hata hivyo, alidumu kwenye benchi kwa siku 80, kabla ya kufungashiwa virago akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi mbili tu za Ligi Kuu Bara.

Ikiwa ni miaka 13 imepita, kwa sasa Mbelgiji huyo ni miongoni mwa makocha wenye ‘CV’ kubwa katika soka la Afrika kutokana na kazi nzuri aliyoifanya tangu alipoondoka Yanga.

Alipoajiriwa kuinoa Gambia mwaka 2018, Saintfiet aliikuta timu ya taifa hilo ikiwa kwenye hali mbaya. Haikuwa imeshinda mchezo wowote ndani ya miaka mitano.

Licha ya ugumu huo, haikumzuia kocha huyo kufanya maajabu ya kuiwezesha Mali kufuzu kwa mara ya kwanza fainali za AFCON.

Alifanya hivyo mwaka 2021, ambapo Gambia ilifika robo fainali, na mwaka 2023 walipoishia hatua ya makundi.
Tangu alipoajiriwa kuliongoza benchi la ufundi la Mali, Saintfiet ameendeleza maajabu yake. Ameifanya timu hiyo kuwa tishio katika michezo yake ya hivi karibuni.

Katika mechi 13 alizokaa kwenye benchi, timu hiyo imeshinda nane, sare nne na kufungwa moja pekee, licha ya kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani.

Je, ni wakati wa Saintfiet kutimiza ndoto ya muda mrefu waliyonayo mashabiki wa soka nchini Mali?
Katika fainali za AFCON za mwaka huu, Mali iko Kund A, ikiwa na wenyeji Morocco, Zambia na Comoro. Ndoto yao ni kutwaa ubingwa baada ya kufika fainali mara moja (1972).

Akizungumzia fainali hizo na aina ya Kundi lao, Saintfiet anasema: “Tunapaswa kuelekeza nguvu na akili katika kila mchezo, naamini hali ya hewa, miundombinu na viwanja vitakuwa rafiki.

“Naziona timu zote za Kundi A zikiwa na nafasi ya kuvuka makundi. Kwa upande wetu, lengo ni kufika nusu fainali. Nilisema hilo wakati nasaini mkataba wangu, ingawa nafahamu haitakuwa rahisi.”

Saintfiet ameshaita kikosi chake cha wachezaji 28 atakaokwenda nao katika fainali za AFCON. Miongoni mwa mastaa alionao ni kiungo wa Tottenham, Yves Bissouma.

Mbali ya huyo, pia kikosi chake kina nyota kadhaa wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya, wakiwamo Amadou Haidara (RB Leipzig), Nene Dorgeles (Fenerbahce) na Moussa El Bilal Toure (Besiktas).

Pia, hata wanaocheza Afrika, wanazitumikia klabu kubwa, akiwamo kiungo wa kiwango cha juu katika kikosi cha Al Ahly ya Misri, Aliou Dieng.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img