3.9 C
New York

Abou Mayalla; Kipa wa viwango Comoro anayeitaka jezi Taifa Stars

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

ABOUBAKAR Mayalla ni miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiamini ni suala la muda tu kuitwa kuitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Kwa sasa, Mayalla ni mlinda mlango wa kikosi cha kwanza katika klabu ya Amical Clube, ambayo huu ni msimu wake wa pili Ligi Kuu ya Comoro.

Hata hivyo, safari yake ya soka ilianzia hapa Tanzania, akitumikia klabu kadhaa za ‘mchangani’, kabla ya kuchukuliwa na kituo cha kuibua na kukuza vipaji (academy) cha nchini Uganda msimu wa 2015-16.

Katika mahojiano maalumu na GAZETINI, Mayalla anasema: “Nilipotoka Uganda mwaka 2016, nilirudi Tanzania na kusajiliwa na Abajalo FC, wakati huo ikishiriki Ligi Daraja la Pili, ambapo nilitumikia kwa miaka miwili.”
Atimkia Msumbiji, atwaa ubingwa.

Akiwa Abajalo FC ya Sinza mwaka 2018, Mayalla alipata dili la kucheza soka la kulipwa nchini Msumbiji. Ilikuwaje? Anasema:

“Januari, 2018, kuna kocha anaitwa King Juto alikuja kutafuta wachezaji, akiwamo kipa, ili waende Msumbiji. Akawa anakuja mazoezini kunitazama, alivyoridhika na uwezo wangu, viongozi wa Abajalo wakaniruhusu niende.”

Hatimaye, Mayalla alisajiliwa na Benfica De Milamba FC ya Ligi Daraja la Pili (Provincial Ligue) na kuiwezesha kutwaa ubingwa katika msimu wake wa kwanza (2018-19).

“Wakati fulani, changamoto kubwa niliyokuwa nakutana nayo ni lugha ya Kireno, ingawa katika baadhi ya maeneo wanazungumza Kimwani, ambacho hakitofuani sana na Kiswahili,” anasema.

Kutokana na kiwango chake bora langoni, Mayalla alipanda na kuingia Daraja la Kwanza (Segunda Ligue) baada ya kusajiliwa na Aguia Azul De Nampula mwaka 2022.

Coromo marufuku wachezaji ‘kuroga’

Katika mahojiano yake na GAZETI, Mayalla anasema masilahi ndiyo sababu kubwa ya kujiunga na timu yake ya sasa, Amical Clube, baada ya miaka minne ya kukipiga Msumbiji.

“Lakini pia, kwangu ni kama nimepanda zaidi, maana sasa nacheza Ligi Kuu, tofauti na niliyokuwa Msumbiji. Pia, kwa sasa nipo chini ya wakala, tofauti na mwanzoni, ambapo nilikuwa najipambania mwenyewe,” anasema.

Mayalla anazungumzia pia tofauti kubwa ya maisha ya soka kati ya mataifa mawili hayo. “Huku Comoro wameweka mbele zaidi imani ya Mungu. Kabla ya mechi, zinasomwa sana dua, wanaitwa mashekh kwa ajili hiyo tu. Pia, wachezaji mnahimizwa kuswali, wachezaji hawaruhisiwi kufanya ushirikina,” anaongeza.

Wakati huo huo, kipa huyo ambaye bado familia yake ipo Tanzania, anafichua ilivyokuwa ngumu kwake kujihakikishia namba katika ‘first eleven’ ya timu hiyo.

“Katika mechi mbili za mwanzo, sikupata nafasi. Nikawa kipa wa akiba. Nikaongeza jitihada mazoezini na Nashukuru Mungu, nilianza kuwa chaguo la kwanza katika mechi ya tatu na hadi leo imekuwa hivyo,” anasema Mayalla.

Aitaka jezi Stars, amtaja Diara

Kuitumikia timu ya taifa ni ndoto ya kila mchezaji katika ulimwengu wa soka. Ipo hivyo pia kwa Mayalla, akisema anaamini ni suala la muda na kumuomba Mungu ili kutimiza ndoto yake hiyo.

“Kila kitu ni muda. Binadamu unapanga mipango yako, Mungu naye anapanga. Naendelea kupambana na huenda siku yangu itafika ‘Insha-Allah’,” anasema Mayalla.

Aidha, anatoka wito kwa benchi la ufundi la Stars akiliomba kufuatilia kwa kina maendeleo ya wachezaji wanaocheza soka nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, Mayalla anaiambia GAZETI kuwa Djigui Diara ndiye kipa bora zaidi kwake. “Uwezo wake wa kucheza kwa miguu, kujiamini kwake, na namna anavyowasiliana na mabeki wake, Diarra kwangu ndiye kipa bora zaidi,” anasema Mayalla.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img