13.8 C
New York

Morice Abraham; Kivuli cha ‘Miquissone’ kinachoipa jeuri Simba

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA siku za hivi karibuni, jina la Morice Abraham limekuwa kwenye mijadala ya soka hapa nchini na kwa sasa ni kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na ubunifu wake kwenye eneo la ushambuliaji.
Katika mechi anazoingia akitokea benchi, kasi na uwezo wake kutengeneza nafasi vimekuwa chachu ya uhai wa Simba na hata kuiwezesha kupata ushindi.
Ni kutokana na uwezo wake huo, Abraham kwa sasa ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, akiitwa mara kwa mara katika siku za hivi karibuni na kupata nafasi ya kucheza.
Abraham ni zao la kituo cha kuibua na kukuza vipaji vya soka cha Alliance ya jijini Mwanza na alikuwa nahodha wa kikosi cha Serengeti Boys katika fainali za AFCON kwa vijana wa umri huo mwaka 2019.
Fadlu ampeleka Simba
Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’ waliinasa saini yake wakati wa usajili wa dirisha kubwa, mwaka huu, baada ya wiki kadhaa za kufanya mazoezi chini ya kocha Fadlu Davids.
Abraham aliyezaliwa mwaka 2003, alitua Simba akitokea Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia aliyojiunga nayo mwaka 2021 na kusaini mkataba wa miaka minne.
Nyota huyo alijiunga na Simba akiwa amehusika katika mabao sita ya Spartak Subotica msimu wa 2024-26 na alikuwa miongoni mwa nyota watatu wapya wa mwanzo kusajiliwa na Fadlu baada ya Allasane Kante na Rushine De Reuck.
Miquissone mpya Simba?
Kutokana na uchezaji wake, Abraham anafanana kwa kiasi kikubwa na winga wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Msumbiji, Luis Miquissone.
Kama alivyokuwa Miquissone misimu kadhaa iliyopita, Abraham ameonesha uwezo mkubwa wa kumiliki na kukokota mpira, kupiga pasi na kufunga mabao.
Pia, Abraham ni aina ya washambuliaji wanaopenda kuwafuata mabeki, sifa nyingine kubwa aliyomfanya Miquissone kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba.
Mbali ya hiyo, sifa nyingine ya Abraham, kama ilivyokuwa kwa Miquissone, ni uwezo wa kupiga mashuti ya mbali, uwajibikaji na kujituma ndani ya uwanja.
Udhaifu wake
Huenda wengi waliofuatilia mechi alizocheza akiwa Simba na Taifa Stars wakawa wameona kuwa Abraham amekuwa akichelewa mara kadhaa kufanya maamuzi ya aidha kutoa pasi na kufanya jaribio la kufunga.
Pia, kwa sasa anaweza akawa na mtihani wa kuboresha upigaji wake wa mashuti kwani mara nyingi majaribio yake yamekuwa yakiishia nje ya lango au kuwa dhaifu.
Ataendeleza moto wake?
Licha ya kiwango bora alichonacho, changamoto kubwa aliyonayo Abraham ni kuweza kuepuka presha na kuwa na mwendelezo wa kile anachokifanya sasa ndani ya uwanja.
Katika miaka ya hivi karibuni, soka la Tanzania limeshuhudia vipaji vingi vya soka vikiibuka lakini vikikosa mwendelezo wa viwango na kujikuta vikipotea ndani ya muda mfupi.
Hivyo, ni jukumu la Abraham kuhakikisha anajilinda na mazingira ya ‘kulewa sifa’ ili kuepuka kuangukia kwenye shimo lililomeza vipaji vingi vya wachezaji wazawa.
Kwa umri wake, bado ana nafasi kubwa ya kutimiza ndoto zake za kucheza soka barani Ulaya na kuzisaidia Simba na Stars katika michuano ya kimataifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img