23.2 C
New York

Yanga, Simba na vita ya Bil. 9/- za Caf

Published:

Na Mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuingia hatua ya makundi, sasa klabu za Simba na Yanga zimesogelea utajiri wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wako Kundi B wakiwa na Al Ahly (Misri), AS FAF (Morocco) na JS Kabylie (Algeria).
Simba waliofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, wako Kundi D lenye Esperance de Sportive (Tunisia), Atletico Petroleos de Luanda (Angola) na Stade Malien FC (Mali).
Katika kila kundi, kwa mujibu wa kanuni na Sheria za mashindano hayo, ni timu mbili pekee zitakazoshika nafasi za juu ndizo zitakazokata tiketi ya kuingia hatua inayofuata ya robo fainali.
Msimu huu, kwa mara ya kwanza, bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Dola za Marekani 4,000,000 (zaidi ya Sh bil. 9 za Tanzania).
Ifahamike kuwa dau hilo ni ongezeko la asilimia 40, ukilinganisha na msimu uliopita (2024-25), ambapo bingwa aliondoka na Dola 2,500,000 (zaidi ya Sh bil.6).
Katika michuano mwingine ya Kombe la Shirikisho Afrika, Tanzania inawakilishwa na klabu mbili za Ligi Kuu, Singida Black Stars na Azam FC.
Singida BS, mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, wameangukia Kundi C, ambalo lina CR Belouizdad (Algeria), Stellenbosch FC (Afrika Kusini) na AS Otoho (Congo Brazzaville).
Azam, ambao hii ni mara yao ya kwanza kuingia hatua ya makundi, kama ilivyo kwa Singida BS, wamepangwa Kundi B lenye Wydad AC (Morocco), AS Maniema (DR Congo) na Nairobi United (Kenya).
Safari hii, kama ilivyo kwa Ligi ya Mabingwa, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe, ameongeza kwa asilimia 40 kitita cha bingwa.
Kwamba badala ya Dola 1,250,000 kama ilivyokuwa msimu uliopita, safari hii bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika atalamba Dola 2,000,000.

Related articles

Recent articles