20.3 C
New York

Kwanini Yanga wamemfungashia virago Folz?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA sasa benchi la ufundi la Yanga lipo chini ya kocha msaidizi raia wa Malawi, Patrick Mabedi, ambaye aliajiriwa hivi karibuni.
“Uongozi wa Yanga unamshukuru kocha Roman Folz kwa mchango wake ndani ya klabu yetu na unamtakia kila la heri katika majukumu yake yajayo,” imeeleza taarifa ya Yanga.
Uamuzi wa klabu hiyo kumfungashia virago kocha huyo raia wa Ufaransa umekuja zikiwa ni saa chache tu baada ya kufungwa bao 1-0 na Silver Strikers katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Swali ni je, kipi kilichomponza Folz, ambaye amedumu Jangwani kwa miezi minne pekee tangu alipojiriwa Julai 14, mwaka huu?
Kiwango cha timu
Kwa takimu za ushindi, kocha huyo msaidizi wa zamani wa Mamelodi Sundowns hakufeli Yanga. Katika mechi sita, alishinda nne, sare moja na kufungwa moja. Ni takwimu nzuri kwa kocha mpya.
Hata hivyo, kile ambacho hakuonekana kufaulu, ni kuifanya Yanga icheze kwenye kiwango cha kuvutia.
Kwa miezi minne aliyokaa kwenye benchi la ufundi, Folz alishindwa kuifanya Yanga icheze katika kiwango chake bora, kama ilivyokuwa chini ya makocha waliopita.
Ungeweza kuiona Yanga ya Folz ikikosa ‘movement’ nzuri wakati wa kutengeneza shambulizi, pia ikikosa muunganiko kwenye eneo la mwisho.
Mbaya zaidi, kiwango cha Yanga hakikuonekana kuimarika kutoka mchezo mmoja na mwingine, jambo lililozidi kumpa wakati mgumu kocha huyo.
Presha ya mashabiki
Katika mechi zake chache za awali, mashabiki wa Yanga walionekana kuanza kutilia shaka uwezo wa Folz na wakati mwingine kushinikiza atimuliwe.
Kama itakumbukwa, hata baada ya kushinda mechi nne mfululuzo, bado walimzomea na kusema afukuzwe baada tu ya kufungwa na Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine.
Baada ya mchezo huo, Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alikiri kusikia kilio cha mashabiki na kuahidi kuwa uongozi wa klabu hiyo utafanyia kazi.
Hivyo, hatua ya Folz kufutwa kazi inaweza kutafsiriwa kuwa ni uongozi wa Yanga kutimiza ahadi ya kufanyia kazi malalamiko ya mashabiki wake.
Matarajio ya Yanga
Kwa kiwango cha timu chini ya Folz, ni wazi Yanga ilikuwa ikipishana na matarajio ya uongozi, wanachama na mashabiki kwa ujumla.
Yanga, kwa miaka ya hivi karibuni, imekuwa na kiu ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika).
Baada ya kunusu robo fainali msimu wa 2023-24, ndoto za Yanga kwa upande wa Ligi ya Mabingwa ni kufika nusu fainali au kutwaa ubingwa.
Kwa upande wa Shirikisho, tayari walishafika fainali (2022-23) na sasa matarajio ni kulibeba taji la michuano hiyo. Ni katika matarajio hayo, Yanga haiwezi kutimiza ndoto hizo ikiwa kwenye kiwango kibovu ilichokuwa nacho chini ya kocha Folz.
Ligi ya Mabingwa, kama ilivyo pia kwa Kombe la Shirikisho, ni michuano inayohitaji ubora mkubwa wa ndani ya uwanja, ambao haukuonekana kwa Yanga ya kocha huyo.
Nabi kurejea Jangwani?
Mabedi ameyabeba kwa muda majukumu ya kocha mkuu lakini haitashangaza endapo Yanga watavutiwa na kazi yake na kumpa ajira ya moja kwa moja.
Pia, mabosi wa ‘Timu ya Wananchi’ wanafahamu kuwa kipenzi cha mashabiki wao, Nasreddine Nabi, hana kazi kwa sasa baada ya kuachana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Iko wazi kuwa Yanga wana historia nzuri na kocha huyo raia wa Tunisia, wakikumbuka kuwa ndiye aliyewapeleka kwa mara ya kwanza hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img