Na mwandishi wetu, Gazetini
HUKU idadi ya vijana wanaovuta shisha ikifikia milioni 15 duniani kote, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limezionya kampuni zinazotengeneza bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa WHO, matumizi ya shisha yameongezeka zaidi kwa vijana wadogo wenye umri kati ya miaka 13 na 15, wengi wao wakiwa kwenye mataifa yanayofanya vizuri kiuchumi.
Hata hivyo, kile kilichoishutua zaidi WHO ni kwamba ongezeko la watumiaji wa kundi hilo ni mara tisa ya watu wazima.
Kutokana na hilo, tayari Serikali ya Uingereza imepanga kupitisha sheria itakayosimia udhibiti wa matumizi ya shisha kwa watoto.
“Vijana wanaonekana kuwa watumiaji wakubwa kuliko watu wazima. Majibu haya yanaonesha kuwa kampuni za bidhaa hizi zinalenga zaidi watoto na vijana,” inaeleza ripoti ya WHO.
“Shisha zinachukua nafasi kubwa ya matumizi, ukilinganisha na urahibu wa ‘nicotine’,” anasema Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya WHO, Etienne Krug.
Kwa upande mwingine, kasi ya ongezeko la watumiaji wa shisha imeonekana kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya tumbaku.
Takwimu ziko wazi, zikionesha kuwa watumiaji wa tumbaku duniani wamepungua kutoka bilioni 1.38 mwaka 2000 hadi bilioni 1.2 mwaka 2024.
“Mamilioni ya watu wameacha na hawatumii kabisa tumbaku, inafaa kuzipongeza nchi zilizochukua hatua na kufanikisha maendeleo hayo,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Taasisi inayoendesha kampeni za kupinga matumizi ya sigara ya Action on Smoking and Health, Hazel Cheeseman, anasema:
“Kasi ya matumizi ya shisha nchini Uingereza imesababishwa na nia ya kuachana na uvutaji wa sigara. Lakini, kwa miaka mingi ya hivi karibuni, matumizi ya shisha yamekuwa makubwa zaidi, lazima hatua zichukuliwe.”
Published:


