14 C
New York

Singida Black Stars na safari yao ya kibabe CAF

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuisukuma nje ya mashindano Rayon Sports ya Rwanda, Singida Black Stars wameonga mbele na kuingia hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa wanajiwinda kuikabili Flambeau du Centre ya Burundi.
Ni safari nyingine ya timu za Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya Simba kufika fainali msimu uliopita ilipofungwa na RS Berkane ya Morocco.
Msimu huu, Singida Black Stars, licha ya ugeni wao katika michuano ya kimataifa, walivuka raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Rayon Sports na sasa wana kibarua kingine kigumu mbele ya wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki, Flambeau du Centre.
Ili kuingia hatua ya makundi, watalazimika kuitoa Flambeau du Centre iliyoingia raundi hii ya pili kwa kuing’oa Al Akhdar ya Ligi Kuu nchini Libya.
Ikianzia katika uwanja wa nyumbani mjini Bujumbura, Flambeau du Centre ilipata ushindi wa mabao 2-1, kabla ya kuondoka na sare ya bao 1-1 ilipokwenda ugenini.
Timu hiyo inasaka rekodi ya kuwa timu pekee ya Burundi kuingia makundi ya michuano ya CAF tangu Vital’O ilipofika fainali ya Kombe la Washindi (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) mwaka 1992.
Hata hivyo, Singida Black Stars wanajivunia ubora na uzoefu mkubwa wa benchi lao la ufundi, hasa baada ya mabosi wa timu hiyo ‘kuvunja kibubu’ na kumuajiri aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.
Gamondi mwenye umri wa miaka 61, ni miongoni mwa makocha wanaolijua vizuri soka la Afrika, achilia mbali michuano ya CAF, kutokana na klabu nyingi alizofundisha kwa nyakati tofauti.
Kwa kuzitaja chache, kocha huyo wa kimataifa wa Argentina amewahi kuzinoa Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), CR Belouizdad na USM Alger (Algeria), na Esperance de Tunis (Tunisia).
Wakati huo huo, Singida Black Stars inaweza kujivunia aina ya kikosi ilichonacho msimu huu. Mbali ya kuwa na wachezaji wengi wa kigeni, ujio wa Khalid Aucho na Clatous Chama umekiongezea ukomavu kutokana na uwezo na uzoefu wa viungo hao katika michuano ya kimataifa.
Si tu viwango vyao, bali hata mafanikio yao wakiwa na Simba na Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho yanaweza kuwa msaada mkubwa wa kisaikolojia kwa wachezaji wengine wa Singida Black Stars.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img