22 C
New York

Hawa hapa wapinzani wa Yanga raundi ya pili CAF

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Yanga, nao wametinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni baada ya kuing’oa Wiliete Benguela ya Ligi Kuu nchini Angola.
Yanga walianzia ugenini kwa ushindi wa mabao 3-0, kabla ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa jijini Dar es Salaam.
Sasa, ‘Timu ya Wananchi’ itavaana na Silver Strikers katika raundi ya pili, ambayo mshindi wa matokeo ya jumla atakata tiketi ya kuingia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba, Yanga wataanzia ugenini kati ya Oktoba 17-19, kabla ya kurudi nyumbani kati ya Oktoba 24-26, mwaka huu.
Silver Strikers ya Malawi ilifika hatua hii kwa sheria ya bao la ugenini dhidi ya Elgeco Plus ya Madagascar. Ikianzia ugenini, ilipata sare ya bao 1-1, kabla ya kulazimishwa suluhu (0-0) katika mechi ya nyumbani.
Timu hiyo iliyoanzishwa na wafanyakazi wa Benki ya Malawi mwaka 1977 ikiitwa ‘The Bankers’ wakati huo, ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Malawi msimu uliopita.
Kwa upande mwingine, Silver Strikers inayomiliki uwanja unaopokea mashabiki 18,000 ni miongoni mwa klabu zenye historia nzuri katika soka la Malawi, ikiwa imetwaa mara tisa taji la Ligi Kuu.
Endapo itaitoa Yanga, itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa timu hiyo yenye maskani yake mjini Blantyre kuingia hatua ya makundi baada ya kufanya hivyo msimu wa 2023–24 na 2024–25.
Kwa upande wa Ligi Kuu msimu uliopita, Silver Strikers walinyakua ubingwa baada ya kuukosa kwa miaka 11. Ubingwa ulikuja baada ya ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Premier Bet Dedza Dynamos.
Ni kwa maana hiyo, wakiwa na pointi 67, walihitimisha ubabe wa Nyasa Big Bullets iliyokuwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Malawi kwa misimu mitano mfululizo.
Anayekinoa kikosi cha Silver Strikers ni nyota wa zamani wa Nyasa Big Bullets na timu ya taifa ya Malawi, Peter Mponda, ambaye huo ulikuwa ni ubingwa wake wa kwanza akiwa kocha mkuu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img