Na Mwandishi Wetu, Gazetini
AKIWA na umri wa miaka 82, Joe Biden aliondoka madarakani na kumpisha Donald Trump aliyeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kurejea Ikulu kuiongoza Marekani.
Hata hivyo, tofauti na watangulizi wake, Biden amejikuta akiishi maisha yaliyotawaliwa na madeni mengi baada ya kuondoka madarakani. Mbaya zaidi, ukiweka kando madeni mengi aliyonayo, kwa umri wake, imekuwa ngumu kwa Biden kupata kazi zingine za kumuingizia kipato, tofauti na ilivyokuwa kwa Barack Obama na wengineo.
Kwa mujibu wa taarifa, Biden aliondoka madarakani akiwa na deni la mkopo wa kati ya Dola 250,000 na 500,000, ambapo riba yake ni asilimia 3.375.
Alichukua mkopo huo katika Benki ya TD mwaka 2013, wakati huo Biden akiwa na umri wa miaka 70 na atalipa kwa kipindi cha miaka 30.
Ikumbukwe, alichukua Dola 250,000 alipokuwa likizo nyumbani kwake Delaware mwaka 2022, wakati huo akiwa tayari ni Rais wa Marekani.
Wakati huo huo, Biden anakabiliwa na deni la mkopo wa Dola 50,000 aliochukua katika moja ya benki, ikielezwa kuwa riba yake ni asilimia 5.
Vilevile, ripoti zinaweka wazi mkopo mwingine wa Dola 15,000, ambao riba yake ni asilimia 8 na mwanasiasa huyo anapaswa kuumaliza kabla ya mwaka 2028.
Huku madeni yakiwa ni makubwa kiasi hicho, kampuni ya CelticCapri Corp, ambayo alianzisha mwaka 2017 ili iwe inakusanya mapato yatokanayo na mauzo ya vitabu vyake, nayo haijaonekana kuvuna fedha nyingi.
Katika mwaka wake wa mwisho madarakani, Biden aliambulia Dola 3,100 pekee katika mirabaha ya vitabu vyake vinne, kikiwamo kinachofahamika kwa jina la ‘JOEY – The Story of Joe Biden’ na ‘Willow the White House Cat’.
Licha ya mkataba wake wa Dola milioni 10 na kampuni ya uchapishaji vitabu ya Hachete, bado Biden ameachwa mbali na Obama, ambaye biashara ya uandishi ilimpa Dola milioni 60 baada ya kuondoka madarakani.
Nje ya uandishi wa vitabu, watangulizi wake, akiwamo Bill Clinton, wameweza kuvuna fedha nyingi kupitia hotuba zao mbalimbali. Mathalan, Clinton alipata zaidi ya Dola milioni 100.
Akihojiwa na Gazeti la Daily Mail, mmoja ya wanachama waandamizi wa Chama chake cha Democrats, anasema Biden si mwanasiasa mwenye mvuto mkubwa mbele ya wananchi, hivyo hawezi kupata hotuba za kumpa fedha nyingi kwa sasa.
“Siyo mwanasiasa ambaye watu watashawishika kwenda kwa wingi katika mikutano anayozungumza. Ni tofauti na wenzake wengi,” anasema.
“Hivyo, sioni wafadhili au taasisi nyingi zikimtafuta kwa kazi hiyo. Siyo kwa sababu Trump yuko madarakani …”
Kwa upande mwingine, Biden haonekani kuwavutia hata wenzake wa Chama cha Democrats, ambao huenda wangempa hotuba za kumuingizia fedha nyingi. Ni kwa kuwa aliwahudhi baada ya kuonesha nia ya kutaka kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
“Wengi wetu ndani ya Democrats hatukufurahia uamuzi wake wa kutaka kugombea tena. Kwa hiyo, ni wachache tu wanaoshawishika kumsaidia kiuchumi wakati huu akiwa nje ya urais,” anasema mmoja ya wanasiasa wa Chama hicho.


