LONDON, Uingereza
KLABU ya Chelsea imefunguliwa mashitaka 74 yanayohusu malipo yake kwa mawakala wa wachezaji.
Mashitaka hayo ya Chama cha Soka cha England (FA) ni juu ya malipo ya mawakala kuanzia mwaka 2009 hadi 2022.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mashitaka hayo yamejikita katika usajili wa wachezaji na malipo waliyopokea mawakala wao.
Hata hivyo, makosa yalifanyika wakati huo Chelsea ikiwa chini ya bilionea Roman Abramovich, ambaye aliiuza klabu hiyo kwa tajiri wa Marekani, Todd Boehly.
Miongoni mwa adhabu zinazoweza kuikumba klabu hiyo ya Magharibi mwa London ni kutozwa faini, kufungiwa kusajili au kukatwa pointi.
Kwa upande wake, FA imeliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa inaendelea na uchunguzi.
Mwaka 2023, Chelsea ilitozwa faini ya Pauni milioni 8.6 na Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kwa kosa la kuwasilisha taarifa za fedha zisizo sahihi.
Published:


