Na mwandishi wetu, Gazetini
RAIS wa Marekani, Donald Trump, anajaribu kuingia kwenye historia ya kumaliza mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Tujikumbushe; kiongozi huyo alikuwa na ndoto hiyo tangu akiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, akisema angemaliza vita hivyo muda mfupi tu baada ya kungia madarakani.
Akizungumza Agosti 18, mwaka huu, alisema anajivunia historia yake ya kuwa msuluhishi wa migogoro mingi, hivyo ni suala la muda tu kuziona Urusi na Ukraine zikiweka silaha chini na kupeana mikono.
Je, ni migogoro ipi aliyowahi kusuluhisha, kiasi cha Rai Trump kuonekana anatosha kuwa mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel? Makala haya yanachambua.
Mosi, ni vita ya siku 12 kati ya Israel na Iran. Ilianza Juni 13, mwaka huu, baada ya Israel kuishambulia Iran. Kama haijasahaulika, vita ilikoma siku chache tu baada ya Serikali ya Trump kuingilia kati kwa kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran.
Pili, kuna vita ya Pakistan na India. Mataifa hayo yamekuwa na uhasimu wa miaka mingi lakini hali ilikuwa mbaya zaidi Mei, mwaka huu, baada ya Pakistan kufanya mashambulizi mjini Kashmir.
Trump aliingilia kati na kuwaita kwenye meza ya mazungumzo viongozi wa India na Pakistan na hatimaye kufanikiwa kumaliza vita ya siku nne.
Baadaye, Pakistan ilimshukuru Trump na hata kupendekezwa kupewa tuzo maarufu ya Amani ya Nobel Peace, ikimtaja kuwa ni mwanadiplomasia wa kiwango cha juu duniani.
Tatu, Trump alimaliza uhusiano mbaya kati ya Rwanda na majirani zao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), licha ya kwamba bado mataifa hayo ‘hayaaminiani’.
Chanzo cha mgogoro ni Rwanda kushutumiwq kuwa imekuwa ikiwafadhili waasi wa Kundi la M23 wanaoshikilia maeneo yenye utajiri wa madini Mashariki mwa DRC.
Kupitia Trump, wawakilishi wa pande mbili hizo walikutana jijini Washington mwishoni mwa mwaka jana na kusaini mkataba wa amani.
Lakini, licha ya jitihada hizo za Trump, bado zipo taarifa kuwa Rwanda na DRC zinaendelea kupigana. “Bado kuna mapigano kati ya Congo na Rwanda,” anasema Profesa wa historia aliyewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Oxford, Margaret MacMillan.
Nne, ni vita ya Thailand na Cambodia. Julai 26, mwaka huu, Trump kupitia mitandao ya kijamii, aliyataka mataifa hayo kuacha mara moja vita iliyokuwa ikiendelea.
Trump alitishia kuziondoshea misaada, pamoja na kuziwekea ushuru mkubwa bidhaa zinazotoka Thailand na Cambodia endapo mataifa hayo yangeendelea kupigana.
Siku chache baadaye, pande mbili hizo zilitangaza kuacha vita iliyokuwa imedumu kwa takribani wiki moja katika maeneo ya mpakani.
Tano, ni vita ya Armenia na Azerbaijan. Agosti 8, mwaka huu, Trump ndiye aliyemaliza mgogoro huo uliokuwa umedumu kwa miaka zaidi ya 40.
Baada ya kumaliza mgogoro huo, pande mbili hizo zilijitokeza na kusema Trump anastahili kupewa tuzo ya Amani ya Nobel.
Sita, haikuwa vita, bali ni mgogoro mkubwa kati ya Misri na Ethiopia juu ya Mto Nile. Trump aliahidi na hatimaye kumaliza mvutano uliokuwa umekosa majibu kwa miaka 12.
Saba, ni mgogoro wa miaka mingi kati ya Serbia na Kosovo. Juni, mwaka huu, mataifa hayo yalikaribia kuingia kwenye vita, kabla ya Trump kuingilia kati na kuzionya.
“Serbia na Kosovo zilikuwa mbioni kuingia vitani, tena vita kubwa. Nilizionya, kwamba Marekani ingeacha kabisa kufanya nazo biashara endapo zingethubutu kupigana. Zikakubaliana kuacha vita,” alisema Trump.
Published:


