CAIRO, Misri
UONGOZI wa klabu ya Al Ahly umemfuta kazi kocha wake raia wa Hispania, Jose Riveiro, ikiwa ni baada ya mechi nne tu za msimu huu wa 2025-26.
Ahly imeshinda moja kati ya mechi nne hizo za mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Misri.
“Ahly inamtakia kila la kheri kocha Jose Riveiro na wasaidizi wake,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo ya jijini Cairo.
Mabingwa watetezi hao walifungua pazia kwa sare ya mabao 2-2 na Modern Sport, wakashinda 4-1 dhidi ya Pharco FC, kabla ya suluhu (0-0) mbele ya Ghazl El Mahalla.
Aidha, mchezo wao wa mwisho ni ule wa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao, Pyramids FC.
Mara ya mwisho kwa vigogo hao wa soka la Afrika kuwa na mwanzo mgumu kwenye Ligi ilikuwa mwaka 2017, ambapo walikusanya pointi nne tu baada ya mechi tatu.
Riveiro mwenye umri wa miaka 49, aliajiriwa Mei, mwaka huu, kwa mkataba wa miaka miwili baada ya Marcel Koller kufungashiwa virago.
Published:


