ISTANBUL, Uturuki
KLABU ya Fenerbahce imetangaza kumfungashia virago kocha wake raia wa Ureno, Jose Mourinho ‘Special One’ ukiwa ni mwaka mmoja tu tangu alipoajiriwa.
Hatua ya kufukuzwa kazi imekuja baada ya Mourinho kuishuhudia timu hiyo ikipoteza mchezo wa ‘play-offs’ ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Benfica.
Mourinho mwenye umri wa miaka 62, aliiwezesha Fenerbahce kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita.
Maisha yake nchini Uturuki yalitawaliwa na matukio mengi ya utata, ukiwamo ugomvi wake na klabu ya Galatasaray.
Itakumbukwa, mabosi wa Galatasaray waliwahi kutishia kumfungulia kesi mahakamani wakidai alitoa kauli za kibaguzi dhidi ya wachezaji wao wenye asili ya Afrika katika mechi iliyomalizika kwa suluhu mwanzoni mwa mwaka huu.
Pia, Mourinho mara zote alikuwa mkosoaji mkubwa wa soka la Uturuki, akielekeza zaidi lawama kwa waamuzi wa Ligi Kuu.
Ni kutokana na lawama nyingi kwa waamuzi, kocha huyo wa zamani wa Chelsea alifungiwa mechi nne, kabla ya adhabu kupungua na kumwachia mbili.
Published:


