LOS ANGELES, Marekani
UTAMADUNI wa kucheza kamari umeonekana kukita mizizi kwa vijana wengi duniani, ingawa sasa utafiti umebaini kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya tabia hiyo na changamoto ya afya ya akili.
Hali ni mbaya zaidi nchini Uingereza, ambapo ripoti ya utafiti wa Serikali inaeleza kuwa asilimia 91 ya watoto na vijana hucheza kamari.
Kwa mujibu wa watafiti wa Hong Kong, China, kucheza kamari ni chanzo cha kukosa usingizi na msongo wa mawazo, ambavyo kwa kiasi kikubwa husababisha changamoto ya afya ya akili.
Utafiti wao ulichunguza vijana 2,592, wakiwamo wanafunzi, ambapo wengi wao, sawa na asilimia 31, walikiri kujihusisha na michezo ya kamari, wakisema hutumia hadi zaidi ya saa tano mfululizo kwa kazi hiyo tu.
Kutokana na kamari, vijana hao walikiri kupata changamoto za msongo wa mawazo, upweke, kukosa usingizi, kupoteza hali ya kujiamini, na hata kufanya vibaya katika masomo yao.
“Utafiti wetu ulibaini kuwa vijana hao hawakuwa na changamoto hizo kabla ya kuanza kujihusisha na kamari,” inaeleza ripoti ya utafiti.
Aidha, utafiti wa Hong Kong umetanguliwa na tafiti zingine zinazoonesha kuwa kati ya watoto nane wenye umri wa miaka 16, watano wanakabiliwa na changamoto ya afya ya akili. Ni takwimu za mwaka 2023, likiwa ni ongezeko la asilimia saba ukilinganisha na mwaka 2017.
Published:


