12.6 C
New York

Reijnders; ‘Fundi’ mpya Etihad aliyeziba pengo la De Bryune

Published:

MANCHESTER, England
KUONDOKA kwa Kevin De Bryune kuliwaachia simanzi mashabiki wa Manchester City lakini ujio wa Tijjani Reijnders ni kama umeanza kuwasahaulisha kila kitu kuhusu Mbelgiji huyo aliyetimkia Napoli majira haya ya kiangazi.
Reijnders, raia wa Uholanzi aliyesajiliwa akitokea AC Milan, alionesha kiwango bora katika mechi ya kwanza ya msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL), Man City ilipopata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wolves.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, si tu aliingia kambani mara moja, bali pia alitoa pasi ya bao (asisti) na kuwa mchezaji wa pili wa Man City (baada ya Sergio ‘Kun’ Aguero) kufanya hivyo katika mchezo wake wa kwanza EPL.
Mbali ya kufunga na asisti, Reijnders aligusa mpira mara 82, wakati huo pia pasi tano tu zikipotea kati ya 57 alizopiga katika mchezo huo.
Kwa ufupi, si tu pengo la De Bryune, bali pia uwepo wa Reijnders uliwasahaulisha mashabiki wa Man City kwamba timu yao haikuwa na Rodri wala Phil Foden katikati ya uwanja.
“Ni mwanzo mzuri. Nimefurahi kufunga, kutoa asisti na kupata ushindi. Ni mwanzo mzuri na tunapaswa kuwa na mwendelezo huo,” alisema Reijnders akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Kwa upande mwingine, aligusia tofauti aliyoiona kati ya EPL na Serie A akisema: “(England) nimeona kasi ni kubwa na ni Ligi ngumu, lakini ni jambo zuri kuwa hapa na kufunga bao katika mechi ya kwanza.”
Wakati huo huo, mpachikaji mabao wa zamani wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Alan Shearer, alimzungumzia Reijnders akisema:
“Alikuwa bora sana (dhidi ya Wolves). Kilikuwa kiwango bora sana kwa mchezaji wa eneo la kiungo. Kasi yake ilimfanya atawale katikati ya uwanja.
“Ni ngumu kukabiliana naye, maana anatembea muda wote. Man City ilibebwa zaidi na uwezo wake wa kuhama maeneo mengi ndani ya uwanja.”
Safari ya ya soka ilianzia katika klabu ya PEC Zwolle ya Uholanzi mwaka 2017, kabla ya kujiunga na vigogo wa soka nchini humo, AZ Alkmaar, mwanzoni mwa mwaka 2018.
Baada ya kupelekwa kwa mkopo RKC Waalwijk msimu wa 2019-20, Reijnders alirejea AZ Alkmaar na kuwa mchezaji muhimu kikosini, akifunga mabao 13 na asisti 15 katika mechi 128.
Makali hayo yaliivutia AC Milan iliyomsajili mwaka 2023. Msimu uliopita, alifunga mabao 10 na kutoa asisti nne. Alizidiwa na Scott McTominay wa Napoli tu kwa upande wa viungo waliochangia mabao mengi Serie A.
Licha ya AC Milan kumaliza msimu ikiwa nafasi ya nane katika msimamo, Reijnders alikuwa wa pili kwa upande wa wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi za mabao.
“Siku zote, huwa najaribu kutafuta nafasi ndani ya boksi, napambana kupata nafasi ya aidha kufunga au kutoa asisti. Nikiwa kama kiungo, mchango wangu kwa timu ni kufunga au kutoa asisti,” alisema staa huyo.
Kwa sasa, Reijnders pia ni mchezaji tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi. Ameshacheza mechi 23, zikiwamo zote sita alizoingia kikosi cha kwanza wakati wa michuano ya EURO ya mwaka jana nchini Ujerumani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img