Na Faraja Masinde, Gazetini
Katika kuhakikisha kuwa inakabiliana na makali ya ukosefu wa ajira, Serikali imepanga kutengeneza ajira za wanawake na vijana milioni 3 kote nchini.
Hayo yamebainishwa Juni 14,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023.
“Ili kupunguza umaskini kwa Watanzania, Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni 3 katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025.
“Hii itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000, sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo 2030.
“Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itatekeleza Schemes ndogo za umwagiliaji kote nchini.Tunataka vijana watoke mjini kuelekea kwenye mashamba ya umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya kuvunia maji ya mvua,” amesema Dk. Nchemba.
Ameongeza kuwa: “Tuna Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na mito mikubwa, kama Malagarasi, Ruvuma, Rufiji, Mara, Pangani, Ruvu nk, haya maji tutayatumia kwenye skimu za Umwagiliaji.
“Kwa ardhi, maji na watu tulio nao, ni jambo la aibu kwa Tanzania kulia shida ya ngano, shida ya mafuta ya kula kwa sababu ya vita vya Ukraine na Urusi, sisi tunayo fursa ya kuilisha Afrika, Ulaya na Asia katika baadhi ya mazao,” amesema Dk.Nchemba.