Mwaka mpya wa masomo nchini Tanzania umeanza tangu Jumatatu Januari 17, 2022 ambapo shule za Elimu Msingi na Sekondari zimefunguliwa.
Upekee ulioshuhudiwa kwa mwaka huu ni kuona kuwa jumla ya wanafunzi wote 907,803 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 wakiwemo wavulana 439,836 na wasichana 467,967 wanaanza masomo.
Hii inamaana kwamba hakutakuwa na wanafunzi watakaochelewa kuanza masomo yao.
Siri ya hayo yote ni kuwa kwa mwaka huu Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekamilisha ujenzi wa madarasa 15,000 ya sekondari.
Madarasa hayo ni kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 Sh Trilioni 1.3 zilizotolwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo serikali ilitumia Sh bilioni 304 kwajili ya kugharamia elimu.
Kwani mbali na madarasa hayo pia kuna mabweni 50 yaliyojengwa katika shule za elimu-msingi 50 kwa ajili ya kusaidi wanafunzi wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeonyesha kuwa Mikoa mitano yenye matarajio ya kupokea wanafunzi wengi zaidi kwa Kidato cha Kwanza ni Dar es Salaam (78,738), Mwanza (68,725), Kagera (50,735), Mara (48,855) na Morogoro (48,515).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI jumla ya wanafunzi walionaotarajiwa kuandikishwa shuleni kwa mwaka wa masomo 2022 ni 3,853,460.
Idadi hiyo inahusisha wanafunzi wa darasa la Awali 1,363,834; darasa la Kwanza 1,581,823 na Kidato cha Kwanza 907,803, ikilinganishwa na wanafunzi 3,631,715 wakiwemo wanafunzi 1,198,564 wa darasa la Awali, wanafunzi 1,549,279 wa darasa la Kwanza na wanafunzi 883,872 wa Kidato cha Kwanza 2021.
Hawa ni wanafunzi wa kwanza kuanza masomo wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani.
Zaidi angalia usanifu wetu.