TANZANIA iko kwenye mfululizo wa kueleza mafanikio yaliyopatikana kwa miaka 60 tangu ilipopata Uhuru wake Desemba 9, 1961.
Katika kuelekea kilele cha miaka 60 ya Uhuru Desemba 9, Serikali kupitia Wizara zake mbalimbali imeendelea kueleza mafaniko yaliyopatikana zikiwamo changamoto kuanzia wakati huo hadi hivi sasa ambapo unaposoma makala haya tayari iko kwenye nchi za uchumi wa kati.
Moja ya wizara nyeti ambazo tayari zimeainisha mafanikio na changamoto zake katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Uhuru ni pamoja na ile ya Madini.
Akiainisha mafanikio ya wizara yake hiyo mapema mwezi huu, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, anasema ndani ya miaka 60 ya Uhuru sekta ya madini imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha biashara na kudhibiti utoroshwaji wa madini nje ya nchi.
“Yapo mengi ambayo tumefanikiwa kuyatekeleza katika sekta hii ya madini, kubwa ni kuimarika kwa biashara ya madini. Jingine kubwa ni kufanikiwa kudhibiti kabisa utoroshwaji wa madini nje ya nchi. Hii kwa sasa tunasema ni zilipendwa kama wanavyosema watoto wa mjini, kwani hakuna tena madini yanayotoroshwa kwenda nje ya nchi na nayejaribu kufanya hivyo basi ni kutafuta umaskini au kwenda jela,” anasema Biteko.
Biteko anasema kuwa kwa sasa hakuna wachimbaji wanaohagaika na kutorosha madini kwani kwa kufanya hivyo ni kuharibu mustakabali wao wa maisha.
“Wito wangu kwa Watanzania, kutorosha madini ni zilipendwa hakuna faida hakuna tija mtu yeyote kwa anaefanya hivyo, kwani atakuwa anatafuta vitu viwili tu kati ya jela au umaskini kwenye maisha yake,” amesema Biteko.
Tweet
Changamoto zipo
Pamoja na kuwapo kwa mafaniko hayo, Waziri Biteko anakiri kuwa zipo baadhi ya changamoto ambazo wizara imekutana nazo katika kipindi cha miaka 60 ikiwa ni pamoja na matokeo ya maendeleo ambapo kwa sasa rasilimali fedha, vitu na watu ni muhimu.
“Naweza kusema kuwa changamoto kubwa zilizopo nikutokana na maendeleo kama ambavyo kwenye maisha ya kawaida tu ukifanikiwa jambo moja utazalisha jambo lingine, kwa mfano sekta inapokuwa inavutia watu wengi kuingia ndio mwanzo wa kuiongezeka kwa fursa kama raslimali fedha, watu na vitu kwa ujumla,” anasema Biteko.
Kuajiri Watumishi wapya
Biteko anasema kuwa pamoja na changamoto hizo zilizopo, lakini anamshukuru kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri watumishi wapya ambapo amedai watapunguza changamoto ya uhaba wa watumishi ulioikabili sekta hiyo muhimu kwa uchumi.
Tija ya kuundwa kwa masoko ya madini
Biteko anasema kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo yameletwa na masoko ya madini. Anafafanua zaidi kuwa ndani ya miaka 60 kumekuwa na masoko mengi ya madini ambayo yamesaidia kuongeza mapato na kwa sasa kuna masoko 102 ambapo makubwa ni 50 na madogo 52.
Faida ya ukuta wa Mererani
Ukuta waongeza mapato ya Tanzanite
Aidha, Biteko anasema kuwa madini ya Tanzanite yameongeza mapato ya serikali kutoka Sh milioni 166 kwa mwaka kabla ya kuwepo kwa ukuta hadi kufikia Sh bilioni 3.9 baada ya ujenzi wa ukuta.
Zaidi kuhudu mafanikio yaliyopatikana katika Wizara hii unaweza kutazama Usanifu wetu hapo juu.