8.3 C
New York

Infographic| Homa ya uti wa mgongo ni nini?

Published:

KWA sasa, ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo ni tishio barani Afrika, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO). Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iko kwenye hali mbaya zaidi, ikielezwa kuwa watu zaidi ya 120 wameshapoteza maisha.

Ripoti za WHO zinaonesha nchi 26 barani Afrika, zikiwamo Senegal na Ethiopia, ziko kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo unaoitwa Meningitis kwa jina la kitaalamu. Hata hivyo, si ugonjwa mgeni, ukitajwa kuua watu zaidi ya 100,000 ulimwenguni kote kwa miaka 20 iliyopita.

Maana ya homa ya uti wa mgongo

Ni uvimbe wa utando laini (meninges) unaozunguka ubongo na uti wa mgongo. Husababishwa na makundi ya vimelea vya Nimonia na Kifua Kikuu, pia virusi aina ya Herpes simplex. Hatari ya kifo huwa kubwa zaidi pindi homa hii inapoletwa na bakteria.

Ni ugonjwa unaoathiri hata watoto, ambapo anaweza kuwa na dalili zifuatazo: Homa kali, kulia mara kwa mara, kusinzia, kuchoka, kukataa kula na uvimbe utosini.

Kuenea, dalili zake

Bakteria wanaoeneza ugonjwa huu huweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia hewa, mate au makamasi, na huchukua siku mbili hadi 10 kwa aliyepata maambukizi kuanza kuonesha dalili.

Dalili ni pamoja na homa kali, kichwa kuuma, kutapika, macho kushindwa kuhimili mwanga (photophobia), kuchanganyikiwa na shingo kukakamaa. Aidha, mgonjwa anaweza kupotea usikivu au ulemavu mwingine wa kudumu na hata kufariki.

Chimbuko

Mlipuko wa kwanza wa ugonjwa huo ulitokea Geneva, Uswis, na hiyo ilikuwa mwaka 1805. Kwa upande wa Afrika, mlipuko wa kwanza unatajwa kuibuka mwaka 1840. Jitihada za WHO ni kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa ifikapo mwaka 2030.

Makundi yaliyo hatarini

Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa afya, watu wenye kinga dhaifu, wakiwamo waathirika wa Ukimwi, wako hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo. Ni kama iliovyo hatari kwa watu wanaoishi katika msongamano (wakimbizi, wasafiri n.k.)

Ni ugonjwa unaotibika

Licha ya ulivyo hatari, uzuri ni kwamba homa ya uti wa mgongo ni ugonjwa unaotibika. Endapo mgonjwa mwenye dalili zilizotajwa, anatakiwa kufika haraka kwa wataalamu wa huduma za afya. Si tu kuwezeshwa kupumua vizuri, pia dawa za kuangamiza vimelea vya homa hii zinapatikana.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img