1.4 C
New York

Rugemalira na msoto wa miaka minne gerezani

Published:

NI miaka minne imepita tangu alipokuwa uraiani na hatimaye leo mfanyabiashara James Rugemalira ameuacha mlango wa gereza baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kumfutia mashtaka yanayomkabili.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kuwa kesi dhidi ya Rugemalira iliitwa mahakamani hapo lakini DPP amewasilisha hati ya kuiondoa chini ya kifungu cha Sheria cha 91 (1) cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Chanzo cha kesi

Kesi dhidi yao ilitokana na sakata la Escrow lililoibuliwa Bungeni mwaka 2014, ambapo ilielezwa kuwa fedha zilizokuwa zimetengwa kwenye akaunti maalum iliyofunguliwa kwenye akaunti ya Benki Kuu (BOT) ‘zilichomolewa’ bila kufuata utaratibu.

Rugemalira na mfanyabiashara mwingine maarufu anayemiliki kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Harbinder Sethi, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu miaka minne iliyopita (Juni 19, 2017), ambapo walisomewa mashitaka sita ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kujipatia fedha kwa udanganyifu, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 358.

Wawili hao walitajwa kutenda makosa hayo Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam, ikielezwa kuwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Mwezi uliofuata (Julai 3, 2017), yaliibuka mashtaka mengine sita na kufikia 12, yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo kimsingi hayatoi nafasi ya kuomba dhamana.

Ilipofika Desemba 20, 2019, aliongezeka mshatakiwa mwingine kwenye kesi hiyo, ambaye ni aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege.

Alivyoomba kuachiwa

Mwanzoni mwa mwaka jana (Februari 13, 2020), Rugemarila aliwasilisha ombi kwa DPP akimwomba kumtoa katika kesi kwa kuwa alishawasilisha nyaraka za watu wanaotakiwa kushtakiwa.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alisema kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa tu, hivyo bado upelelezi wake unaendelea.

Wiki mbili baadaye (Februari 27, 2020), Rugemalira aliwasilisha mahakamani hoja yake hiyo ya kutaka aondoshwe katika kesi ya uhujumu uchumi, kisha Wakili Simon akaomba wawasilishe majibu kwa maandishi wiki chache zijazo (Machi 12, 2020).

Aitwa tena mahakamani

Novemba 9, 2020, itakumbukwa kuwa Rugemalira alitakiwa kuwa mahakama baada ya mahakama kutoa hati ya kuwaita, lakini yeye na washitakiwa wenzake wawili hawakufika.

Ni kipindi ambacho kesi zilikuwa zikisikilizwa kwa njia ya video kutokana na janga la Corona na Wakili wa Serikali, Faraja Nguka, alihoji sababu ya washitakiwa hao kutotii wito huo.

Rugemalira arudi mahakamani

Ilikuwa ni Desemba 19, 2020, ambapo Rugemalira aliiomba mahakama kumfutia kesi yake. Aliwasilisha ombi akisema kesi hiyo imechukua muda mrefu, hivyo anapaswa kuachiwa ikiwa upelelezi dhidi yake hautakuwa umekamilika kufikia Desemba 31, 2020.

Seth aachiwa huru, Rugemalira abaki

Ni Juni 16, mwaka huu, ndipo mtuhumiwa mwenzake, Seth, alipoachiwa huru baada ya kuondoshewa makosa 11 kati ya 12 yaliyokuwa yakiwakabili, huku Rugemalira akiendelea kusota gerezani.

Inaeleweka wazi kuwa hatua hiyo ilitanguliwa na kitendo cha Seth na DPP kuingia makubaliano ya kumaliza kesi. Kumaliza kesi, Seth alikubali kulipa fidia ya Sh bil. 26.9.

Hiyo ya Seth kurudi uraini ilikuja baada ya agizo la mahakama la Februari 25, 2021 kutoa siku 30 kwa washitakiwa hao kukubaliana na DPP ili kumaliza kesi za uhujumu uchumi.

Wakati mwenzao huyo akirejea uraiani, Rugemalira na Mwakandege waliendelea kusubiri hatima yao gerezani kwa kile kilichoelezwa upelelezi dhidi yao haujakamilika.

Alivyokwama Septemba 9

Wiki iliyopita (Septemba 9, 2021), Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah, aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi juu ya mashitaka yanayomkabili Rugemalira na Makandege haujakamilika.

Haijasahaulika kuwa Wakili Ngukah aliyasema hayo siku ambayo hata hivyo washtakiwa hao hawakuletwa mahakamani.

Hatimaye amerudi uraiani

Baada ya miaka minne, Rugemalira amerudi uraiani leo (Septemba 16, 2021), tukio lililoteka hisia za wengi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali, Grace Mwanga, umedai kesi dhidi ya Rugemalira iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa lakini DPP amewasilisha hati ya kuiondoa.

“Hatuna nia ya kuendelea na kesi hii na tunaiomba mahakama imwachie huru mshitakiwa Rugemalira,” alisema Wakili Mwanga, huku ikielezwa kuwa mshitakiwa mwingine, Makandege, atabaki gerezani hadi Desemba 23, mwaka huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img