1.6 C
New York

Visualization| Mlango wa kutokea unavyomuita Arteta

Published:

NI miaka takribani 17 bila ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) na Arsenal wameingia msimu huu wakiwa hawana tena matumaini ya kumaliza ndani ya ‘top four’, achilia mbali suala la kuibeba ‘ndoo’.

Baada ya kufungwa na Brentford mabao 2-0 na kisha kutandikwa mabao 2-0 na Chelsea, mkosi uliendelea kuwaandama Washika Bunduki hao wa jijini London wikiendi iliyopita walipochapwa mabao 5-0 na Manchester City.

Matokeo hayo yameendelea kumuweka pabaya kocha wao, Mikel Arteta, ambaye ni miezi 18 sasa tangu alipotangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Washika Bunduki hao.

Katika mechi sita alizokutana na Pep Guardiola, Arteta amepoteza tano.

Kiwango kibovu

Ukiacha matokeo, Arsenal wameuanza msimu na kiwango kibovu, ambapo katika mechi waliyokuwa nyumbani dhidi ya Chelsea, walifungwa wakiwa wamemiliki mpira kwa asilimia 35 tu dhidi ya 65 walizokuwa nazo wapinzani wao.

Walipokutana na Man City, Arsenal walikuwa kwenye kiwango kibovu zaidi kwani walimiliki mpira kwa asilimia 19 pekee kati ya 81 walizokuwa nazo vijana wa Pep Guardiola.

Kwa dakika zote 90, Arsenal walikuwa na shuti moja pekee (halikulenga lango), huku wenzao wakipiga 25 (10 yalilenga lango). Arsenal hawakuambulia kona, wakati Man City walikuwa nazo 10.

Kwa Arsenal ilivyozoeleka kwa soka la kuvutia, unaweza kuhisi kuna tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi kabla ya gari lao kupoteza uelekeo wake moja kwa moja.

Msimu uliopita ilikuwaje?

Hali ilikuwa mbaya tu. Ikimaliza katika nafasi ya 8, Arsenal ilishinda mechi 18, ikafungwa 13 na kuambulia sare saba. Ikiwa na mabao ya kufunga 55, ilikuwa na idadi ndogo zaidi ukilinganisha na timu saba zilizokaa juu yake.

Hata hivyo, ubora wao ulionekana zaidi kwenye eneo la ulinzi kwani Arsenal ikiwa timu pekee iliyoruhusu mabao machache (39), ukiacha Man City (32) na Chelsea (36).

Usajili wa bei mbaya

Licha ya kutumia takribani Pauni milioni 75 (zaidi ya Sh bil. 240 za Tanzania) katika soko la usajili kuwanasa Albert Sambi Lokonga (kiungo), Nuno Tavares (beki wa kushoto) na Ben White (beki wa kati), Arsenal bado ni ile ile.

Kwa mechi tatu za msimu huu wa EPL, imeshafungwa jumla ya mabao tisa, wastani wa mabao matatu kila mchezo. Mbaya zaidi, haijaona nyavu za wapinzani katika mechi zote tatu, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa misimu yote 118 iliyoshiriki EPL.

Majanga yalianzia ‘pre-season’

Ndiyo. Katika kukiweka sawa kikosi chake kuelekea msimu huu, Arsenal ilicheza mechi za kirafiki sita lakini ilishinda mbili tu, ikafungwa tatu na kutoa sare moja.

Udhaifu wa eneo la ulinzi unaoonekana sasa ulionekana tangu kwenye mechi hizo kwani Arsenal iliruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi zote sita, ikipitisha jumla ya mabao tisa. 

Arteta atapona?

Hata kocha Arteta anaweza kuwa ameshaanza kukosa usingizi akiwa nyumbani kwake, hasa kwa kipindi hiki jina la Antonio Conte linapotajwa pale Emirates.

Mechi ya Man City imekuwa ya 21 kwa Arsenal kupoteza kati ya 61 za Ligi Kuu alizoiongoza timu hiyo. Si wastani wa kuridhisha kwa kocha unayetarajiwa kuipa timu ubingwa wa Ligi Kuu yoyote barani Ulaya.

Msimu uliopita, ilikuwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 46 kuiona Arsenal ikishinda mechi nne tu kati ya 12 za mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya England.

Aidha, ilipomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya nane, ilikuwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 25 kuishuhudia Arsenal ikikosa tiketi ya kushiriki michuano ya Ulaya (Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa).

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img