BISSAU, Guinea-Bissau
NI rasmi sasa Jenerali wa jeshi nchini Guinea-Bissau ameapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo, ikiwa ni siku moja tu baada ya mapinduzi.
Jenerali Horta N’Tam anakuwa rais wa mpito kwa kipindi cha mwaka mmoja, kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, wakosoaji wanaamini mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Jumatano ya wiki hii ni mpango wa Rais aliyemaliza muda wake, Umaro Sissoco Embalo.
Kwamba ameshirikiana na jeshi kusuka mapinduzi dhidi yake ukiwa ni mpango wa kuzuia matokeo endapo atashindwa katika Uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Mpango huu umelenga kuzuia utangazaji wa matokeo,” ilieleza moja ya taasisi za kiraia.
Madai hayo yameibuliwa pia na aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro cha urais, Fernando Dias.
Kwa upande wake, Embalo amekanusha madai hayo akidai kuwa amenusurika majaribio mengi ya serikali yake kupinduliwa.
Guinea-Bissau imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi tisa tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1974.
Published:


