12.7 C
New York

Antoine Semenyo; Mkali wa mabao anayegombewa Ligi Kuu ya England

Published:

LONDON, Uingereza
WINGA wa Bournemouth raia wa Ghana, Antoine Semenyo, atauzwa endapo tu klabu zinazomtaka zitaweka mezani kitita cha Pauni milioni 65.
Semenyo (25), alikuwa kwenye rada za Manchester United na Tottenham tangu wakati wa dirisha kubwa la usajili lililopita lakini alisaini mkataba mpya wa miaka mitano kubaki Bournemouth.
Nyota huyo ni moto wa kuotea mbali msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo ameshafunga mabao sita na kutoa ‘asisti’ tatu katika mechi 11.
Kwa Semenyo, huo ni mwendelezo wa kiwango bora alichomaliza nacho msimu uliopita; mabao 13 katika michuano mbalimbali, yakiwamo 11 ya EPL.
Ukiziweka kando Man United na Tottenham, klabu zingine zinazoimezea mate huduma ya mabao ya staa huyo ni Arsenal, Chelsea, Liverpool na Manchester City.
Arsenal walimkataa akiwa kinda
Akiwa mdogo, Semenyo aliwahi kufika katika ‘academy’ za Arsenal na Tottenham lakini hakuchaguliwa kujiunga nazo, akionekana hana kiwango cha kuzishawishi kumchukua.
Ndipo alipochukuliwa na shule ya vipaji vya soka ya SGS College inayomilikiwa na kocha wa zamani wa Leeds United, Dave Hockaday.
Akitokea hapo, Bristol City ilimuona na kumsajili mwaka 2017 lakini ilimtoa kwa mkopo katika klabu za Bath, Newport na Sunderland ili kuimarisha kikosi chake.
Msimu wa 2020-21, Semenyo alifanikiwa kuingia kikosi cha kwanza cha Bristol, kabla ya kiwango chake kuishawishi Bournemouth iliyomsajili mwaka 2023 kwa ada ya Pauni milioni 10.
Shujaa wa Bournemouth
Tangu mwaka 2023, kiungo wa pembeni huyo amekuwa mchezaji muhimu kwa Bournemouth na mabao yake 11 yaliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa EPL msimu uliopita.
Licha ya kuwauza Illia Zabarnyi, Milos Kerkez na Dean Huijsen, pia ikishindwa kumbakiza kipa wa mkopo kutoka Chelsea, Kepa Arrizabalaga, uwepo wa Semenyo kikosini unaifanya Bournemouth kuendelea kuwa imara uwanjani.
Mbali ya mabao sita na asisti tatu, mshambuliaji huyo ametengeneza nafasi 11, amepiga mashuti 14 yaliyolenga lango, pia akipiga pasi 283.
Kuziba pengo la Salah?
Liverpool inamtazama Semenyo kwa jicho la karibu, ikiamini atawafaa Januari, mwakani, wakati Mohamed Salah atakapokuwa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kuanzia Desemba, mwaka huu.
Federico Chiesa ana uwezo mkubwa wa kuziba pengo la Salah, lakini nyota huyo raia wa Italia amekuwa hatabiriki kutokana na majeraha yake ya mara kwa mara.
Kwa upande mwingine, mabosi wa Liverpool wanamuona Semenyo kuwa ni mrithi sahihi wa Salah, ambaye atakuwa na umri wa miaka 34 ifikapo Juni, mwakani.
Semenyo si mgeni kwa mashabiki wa Liverpool. Aliwafunga mabao mawili ndani ya dakika 12 tu za mchezo wao wa kwanza msimu huu wa EPL.
Kwanini United wanamtaka?
Man United haina makali katika safu yake ya ushambuliaji. Bryan Mbeumo ameonesha kiwango kizuri tangu asajiliwe, lakini bado hajafikia idadi ya mabao na asisti za Semenyo.
Mbaya zaidi, Man United itawapoteza Mbeumo, Amad Diallo na Noussair Mazraoui, ambao watakuwa Afrika kuyawakilisha mataifa yao katika fainali za AFCON.
Kwa upande wa Semenyo, hatakuwa kwenye fainali hizo kwani timu yake ya taifa ya Ghana ilishindwa kukata tiketi.
Guardiola naye ndani
Ukiacha Erling Haaland, ambaye amezifumania nyavu mara 14 msimu huu, Man City ina uhaba wa mabao kutoka kwa washambuliaji wengine.
Kwa Guardiola, faida kubwa aliyonayo Semenyo ni uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi kwenye eneo la ushambuliaji. Winga zote mbili (kulia na kushoto) na wakati mwingine akicheza kama straika.
Isitoshe, Man City itampoteza Omar Marmoush, ambaye naye atakuwa kwenye fainali za AFCON akiiwakilisha timu yake ya taifa ya Misri.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img