PORTO, Ureno
KWA mujibu wake, fainali za Kombe la Dunia za mwakani zitakuwa za mwisho kwake, kisha atatundika daluga. Huyo ni Cristiano Ronaldo.
Ureno inakwenda kwenye michuano hiyo ikiwa inashika nafasi ya sita ya viwango vya ubora wa soka duniani.
Kwa miaka ya hivi karibuni, timu yao ya taifa imekuwa na mafanikio makubwa. Ilibeba taji la fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO) mwaka 2016, kisha ikawa mabingwa wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya (Nations League) mwaka huu.
Kocha ni Roberto Martinez, ambaye aliajiriwa Januari, 2023. Martinez anakuwa kocha wa tatu wa kigeni kuinoa Ureno.
Katika mechi za kufuzu, Ronaldo mwenye umri wa miaka 40 alionesha umuhimu wake kikosini akiifungia timu hiyo jumla ya mabao matano.
Ni wazi atataka kustaafu akiwa ameipa Ureno taji la Kombe la Dunia, ikizingatiwa kuwa mpinzani wake, Lionel Messi, aliibeba mwaka 2022 nchini Qatar.
Mbali ya ‘CR7’, wachezaji wengine tegemeo kwa Ureno kuelekea fainali za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico ni Bruno Fernandes (Man Utd) na Vitinha (PSG).
Msimu uliopita wa Kombe la Dunia, 2022, Ureno iliishia robo fainali. Mwakani itakuwa ni mara ya tisa kwao kushiriki michuano hiyo mikubwa zaidi duniani.
Published:


