PRAIA, Cape Verde
TAIFA hilo linaloshika nafasi ya 68 kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) litashiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia.
‘Blue Sharks’ hawana taji lolote kubwa kwenye historia na kwa sasa kikosi chao kinanolewa na kocha aliyedumu kwenye benchi la ufundi tangu mwaka 2020.
Kwa wafuatiliaji wa soka la Afrika, kocha huyo ni beki wa zamani, Bubista, ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa timu hiyo.
Licha ya kutokuwa na majina makubwa, wachezaji wa kikosi hicho wana ubora wa kuleta ushindani mkubwa msimu ujao wa Kombe la Dunia, akiwamo Dailon Livramento aliyefunga mabao manne katika mechi za kufuzu.
Cape Verde yenye watu 525,000, ni taifa dogo la tatu katika historia ya Kombe la Dunia kukata tiketi ya kushiriki michuano hiyo.
Walijihakikishia nafasi ya kwenda kushiriki mwakani baada ya ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Eswatini, ambao uliwaweka kileleni mwa Kundi D.
Baada ya kukwama kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2002 na 2002, Cape Verde waliitikisa Afrika kwa kufika hatua ya 16 Bora kwenye michuano ya AFCON mwaka 2021.
Msimu uliofuata, 2023, walirudia maajabu yao kwa kufika robo fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika.
Published:


