15 C
New York

Kuelekea Kombe la Dunia 2026: Uholanzi (1)

Published:

AMSTERDAM, Uholanzi
TIMU ya soka ya taifa ya Uholanzi, maarufu kwa jina la ‘Oranje’, nayo itakwenda katika fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani.
Uholanzi inashika nafasi ya saba katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Mwaka 2011, ilikuwa nafasi ya kwanza.
Hao ni mabingwa wa fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO) mwaka 1988 na sasa wako chini ya kocha Ronald Koeman. Amekuwa hapo tangu aliporejea kwenye benchi mwaka 2023.
Watakwenda kwenye fainali zijazo wakiwa na kikosi kilichosheheni wachezaji wenye majina makubwa, wakiwamo Memphis Depay (Corinthians), Cody Gakpo na Virgil van Dijk (Liverpool).
Katika hatua ya kufuzu, Depay aliyewahi kukipiga Manchester United na Barcelona aliibeba kwa kiasi kikubwa safu yao ya ushambuliaji, ambapo alifunga mabao nane.
Baada ya kushindwa kufuzu mwaka 2018, Uholanzi walirejea msimu uliopita wa Kombe la Dunia na kufika robo fainali.
Walifungwa na Argentina katika mchezo uliokuwa na presha kubwa na kushuhudia mwamuzi wa kati raia wa Hispania, Antonio Mateu Lahoz, akitembeza kadi za njano 18 na nyekundu moja.
Uholanzi watakwenda Kombe la Dunia wakiwa na rekodi mbaya wanayotamani kuifuta. Ndiyo timu pekee inayoongoza kwa kuingia fainali nyingi (3) bila kutwaa ubingwa.
Kwa kocha Koeman, mtihani alionao ni kuipa timu hiyo taji kubwa la kwanza tangu ilipotwaa ubingwa wa EURO mwaka 1988.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img