20 C
New York

Wakali wa mabao kufuzu Kombe la Dunia

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
FAINALI za Kombe la Dunia zimekuwa na rekodi nyingi, ikiwamo ile maarufu ya wafungaji bora wa muda wote wa mechi za kuwania tiketi ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Je, unawafahamu wachezaji hao wanaoongoza kwa kuzifumania nyavu katika historia ya mechi za kufuzu michuano hiyo? Makala haya yanachambua.
Chritiano Ronaldo (Ureno)
Mabao 41 katika mechi 52 za kuwania ushiriki wa Kombe la Dunia. Alianza kufunga mwaka 2004, mchezo alioingia kambani mara nne dhidi ya Latvia.
Mwaka 2006, Ronaldo alichangia mabao manne katika mechi tano za kufuzu Kombe la Dunia. Michuano ilipofika, alifunga mengine saba.
Carlos Ruiz (Guatemala)
Nyota wa kimataifa wa Guatemala. Historia ya Kombe la Dunia inatambua mchango wake wa mabao 39 katika mechi 47 za kufuzu.
Kwa miaka 16 ya soka lake, Ruiz amefunga dhidi ya timu kubwa kwenye soka, zikiwamo Canada, Costa Rica na Marekani.
Lionel Messi (Argentina)
Supastaa wa timu ya taifa ya Argentina anayekipiga katika klabu ya Inter Miami ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Kwa upande wa Kombe la Dunia, ana mabao 36 katika mechi 72 za kufuzu michuano hiyo. Mbali ya mabao hayo, Messi ana ‘asisti’ 14.
Ali Daei (Iran)
Mabao 35 katika mechi zake 51 alizocheza za kufuzu Kombe la Dunia. Pia, ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Iran (mabao 110 katika mechi 152).
Katika mabao yake 35 ya Kombe la Dunia, yapo manne aliyofunga dhidi ya Laos, mchezo uliochezwa mwaka 2004.
Robert Lewandowski (Poland)
Kwa miaka mingi, staa huyo wa zamani wa Bayern Munich anayekipiga Barcelona kwa sasa amekuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya timu yake ya taifa ya Poland.
Takwimu ziko wazi, kwamba nyota huyo ameshafunga mabao 34 katika mechi 44 za kuisaisia Bosnia kufuzu Kombe la Dunia.
Edin Dzeko (Bosnia)
Mpachikaji mabao wa zamani wa Manchester City na AS Roma amefunga mara 30 katika mechi 33 za kuwania nafasi ya Kombe la Dunia.
Historia ya Dzeko kufunga katika michuano hiyo ilianza mwaka 2008 alipoingia kambani mara mbili dhidi ya Estonia wakishinda mabao 7-0.
Luis Suarez (Uruguay)
Nyota huyo wa zamani wa Barcelona ameifungia timu yake ya taifa jumla ya mabao 29 katika mechi 64 za kufuzu Kombe la Dunia.
Suarez alifungua akaunti ya mabao kwa kufunga bao moja katika mchezo dhidi ya Bolivia mwaka 2007. Mwaka 2011, alifunga manne dhidi ya Chile. Bao lake la mwisho alifunga dhidi ya wapinzani hao mwaka 2022.
Chris Wood (New Zealand)
Nyota huyo aliyefunga mabao 20 ya mechi za Ligi Kuu ya England msimu uliopita, ana mabao 29 katika mechi 31 za kufuzu Kombe la Dunia.
Wood ameiwezesha New Zealand kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa kufunga mabao tisa.
Sardar Azmoun (Iran)
Straika huyo ni nyota mwingine raia wa Iran, ambaye rekodi zinaonesha kuwa amefunga mabao 29 katika mechi 41 za kuwania tiketi.
Azmoun alianza kwa mabao manne katika mechi tatu za kufuzu Kombe la Dunia za mwaka 2018. Akiwa na umri wa miaka 30 kwa sasa, amefunga mabao nane kuiwezesha Iran kukata tiketi ya fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Karim Bagheri (Iran)
Mshambuliaji huyo wa kimatafa wa Iran, ambaye kwa sasa ameshatundika daluga, ana mabao 28 katika mechi 29 za kufuzu.
Bagheri alianza na mabao saba katika ushindi wa mabao 17-0 dhidi ya Maldives. Ilikuwa ni mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1998.
Pia, aliwahi kupasia nyavu mara sita mwaka 2000, mchezo ambao Iran iliibuka na ushindi wa mabao 19-0 dhidi ya Guam.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img