14 C
New York

Casemiro; Mashine iliyozaliwa upya United, Brazil

Published:

RIO, Brazil
MIEZI 18 iliyopita, beki wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England ‘Three Lions’, Jamie Carragher alikuwa mbele ya kamera za kituo cha televisheni cha Sky Sport akisema Casemiro ‘amekwisha’.
Baada ya kung’ara katika msimu wake wa kwanza Old Trafford, ambapo alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka klabuni hapo, Casemiro alikuwa akipitia kipindi kigumu.
Majeraha ya misuli yalimfanya apoteze kasi yake ndani ya uwanja, hivyo kuonesha kiwango kibovu katika mechi nyingi mfululizo.
Kiwango kibovu zaidi, ambacho ndicho kilichomuibua Carragher na kumtaka Casemiro kustaafu, ni kile alichokionesha katika mchezo dhidi ya Crystal Palace uliochezwa Mei, mwaka jana.
Ni baada ya mchezo huo, kocha Erik ten Hag akachagua kumweka benchi na kuwapa zaidi nafasi viungo Kobbie Mainoo na Scott McTominay.
Zikawepo taarifa nyingi kuwa Casemiro hana tena nafasi ndani ya Man United, hivyo kuhusishwa na klabu za Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Majanga yaliendelea hata katika msimu uliofuata, 2024-25, hasa baada ya Casemiro kuonesha kiwango kibovu katika kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Liverpool. Ten Hag hakurudi tena nyuma. Akawa anamsugulisha benchi.
Mambo yakawa hivyo hata baada ya kocha Ruben Amorim kuajiriwa. Casemiro akaendelea kuwa mchezaji wa benchi akiwatazama Kobbie Mainoo, Manuel Ugarte, Bruno Fernandes na Toby Collyer.
Wakati fulani, Amorim aliweza hata kusema mbele ya vyombo vya habari, kwamba Collyer ni kiungo bora kuliko Casemiro.
Upepo umebadilika ghafla. Kwa sasa, Casemiro anayekaribia umri wa miaka 34, ni mchezaji muhimu kwa Brazil, kama ilivyo katika kikosi cha Man United, wakati huo Collyer akiwa kwa mkopo West Brom.
Kiwango chake bora katika mechi dhidi ya Lyon, bao aliloifunga Athletic Bilbao, na namna alivyoipa wakati mgumu safu ya kiungo ya Man City, ni ujumbe wa kuwaziba mdomo wale walioamini kuwa Casemiro amekwisha.
Ubora wake katika michezo ya hivi karibuni ya Man United umemshawishi kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti, kumrejesha kikosini.
Casemiro amecheza kwa dakika zote 90 za kila mechi tangu aliporejea katika kikosi cha ‘Selecao’, ikiwamo ya siku chache zilizopita walipoifunga Senegal mabao 2-0 jijini London.
Akizungumzia kiwango cha Casemiro katika mchezo huo wa kirafiki, Ancelotti alisema: “Alifanya kazi nzuri sana. Ni mchezaji muhimu sana katika kuleta uwiano tunapokuwa tunamiliki mpira.”
Je, Amorim, anamzungumziaje Casemiro kwa sasa? “Mwanzoni, alikuwa amezidiwa na kila kiungo, hata Toby [Collyer] alimzidi. Lakini alipambana na sasa amerejea timu ya taifa. Wachezaji wengine wanapaswa kumtazama Casemiro …”
Huyo ndiye Casemiro. Kutoka kuwa mchezaji aliyeonekana amekwisha, na sasa ni tegemeo si tu kwa Man United, bali hata kwenye kikosi cha timu yake ya taifa, Brazil.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img