14 C
New York

Neymar kuibukia England Januari?

Published:

RIO, Brazil
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Brazil, Neymar, atakuwa mchezaji huru katika usajili wa dirisha dogo la usajili hapo Januari, mwakani. Mkataba wake na Santos utafikia ukomo Desemba 31, mwaka huu.
Santos hawaoneshi kumuhitaji tena na tayari zipo klabu kadhaa za barani Ulaya zilizoanza kumfuatilia mchezaji huyo, kwa mujibu wa mwandishi wa habari za michezo wa Italia, Fabrizio Romano.
Neymar mwenye umri wa miaka 33, amekuwa akipitia wakati ngumu kurejesha kiwango chake kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara tangu aliporejea kwao, Brazil.
Je, ni klabu zipi zinazoweza kumsajili nyota huyo anayepambana ‘kufufua’ makali yake ili kupata nafasi ya kuiwakilisha timu ya taifa ya Brazil katika fainali za Kombe la Dunia za mwakani?
Chelsea wamekuwa wakimmezea mate kwa muda mrefu. Ni tangu mwaka 2010, ingawa Neymar aliipa kisogo klabu hiyo ya London na kujiunga na Barcelona akitokea Santos.
Hata mwaka 2022, matajiri wa Chelsea walijaribu tena kuinasa saini yake. Je, watamrudia wakati wa usajili wa Januari, ikizingatiwa kuwa Cole Palmer amekuwa akisumbuliwa na majeraha?
Manchester United nayo imetajwa. Kama ilivyo kwa Chelsea, Man United nayo imewahi kuhusishwa mara kadhaa na mshambuliaji huyo wa zamani wa PSG.
Mwaka 2021, mabosi wa Old Trafford walimtaka Neymar na walipomkosa, ndipo walipomrejesha Cristiano Ronaldo kutoka Juventus.
Wakati huo huo, wakali wa Etihad, Manchester City, nao wanahusishwa na mpango wa kumsajili Neymar. Je, atafanya kazi na Pep Guardiola, ambaye amekuwa akimtaja kuwa ni mmoja ya vipaji vikubwa vya soka duniani?
Pia, Liverpool nayo inamtaka Neymar, ingawa inaweza isiwe rahisi kwani klabu hiyo imetoka kutumia Pauni milioni 245 kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Alexander Isak.
Newcastle United, ambayo ina Wabrazil wawili kikosini, Bruno Guimaraes na Joelinton, pia iliwahi kumtaka Neymar na huenda ikajaribu kumsajili ifikapo Januari. Nyota huyo anatajwa kuwa ni kipenzi cha kocha wa klabu hiyo, Eddie Howe.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img