MADRID, Hispania
KABLA ya kusajiliwa na Real Madrid, Kylian Mbappe alishafunga mabao 329 na kutwaa mataji 17 katika maisha yake ya soka.
Ikumbukwe, Mbappe bado ni mfungaji bora wa muda wote wa PSG. Kwa miaka sita alivyokuwa klabuni hapo, alifunga mabao 256 katika mechi 308.
Kwa msimu mmoja tu aliocheza Madrid, takwimu hizo zimeongeka na sasa amefikisha mabao 400 na kutoa ‘asisti’ 169 katika mechi 537 alizocheza katika ngazi ya klabu na timu ya taifa (Ufaransa).
Akiwa na umri wa miaka 26, Mbappe anakuwa mchezaji mdogo zaidi kufikisha mabao 400 tangu lejendari wa Brazil, Pele, alipofanya hivyo akiwa na miaka 23.
Mkali wa ‘hat trick’
Mshambuliaji huyo amefunga ‘hat-trick’ 23 katika michuano nane tofauti, ikiwamo ya Ligue 1, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia.
Ana ‘hat-trick’ nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa amezidiwa na wachezaji watatu pekee; Lionel Messi (8), Cristiano Ronaldo (8) na Robert Lewandowski (6).
Mbappe ndiye mchezaji pekee wa Madrid aliyefunga mabao mengi katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo. Mabao 43 aliyopachika msimu uliopita (2024-25).
Amfunika Henry
Kama hiyo haitoshi, ndiye Mfaransa pekee aliyefunga mabao mengi (31) katika msimu mmoja wa Ligi zote kubwa tano barani Ulaya (England, La Liga, Bundesliga, Ligue 1 na Serie A).
Aliandika historia hiyo msimu uliopita na kumpiku Thierry Henry, ambaye alipachika mabao 30 akiwa na Arsenal msimu wa 2003-04.
Kwa sasa, Mbappe anashika nafasi ya saba katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ufaransa akiwa na mabao 191.
Rekodi yake Ligue 1
Ikumbukwe pia, aliondoka PSG akiwa ni mchezaji pekee katika historia ya soka la Ufaransa kuibeba mara sita mfululizo tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Wakati huo huo, aliondoka Ligue 1 akiwa ndiye mchezaji pekee aliyetwaa mara tano mfululizo tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu hiyo.
Timu alizozifunga mabao mengi
Montpellier ya Ufaransa ndiyo timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi na Mbappe. Mkali huyo ameitungua mara 15 katika mechi 15.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa, timu aliyoinyanyasa zaidi ni Manchester City, ambayo ameifunga mabao saba, ikifuatiwa na Barcelona (6).
Katika mechi 20 alizokutana na timu za England, Mbappe amefunga mabao 10 na kutoa asisti tatu. Ni mechi dhidi ya Man City, Manchester United, Liverpool, Tottenham, Newcastle na Arsenal.
Heshima yake Kombe la Dunia
Mbappe ni mchezaji pekee kuwahi kufunga ‘hat trick’ katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia tangu Geoff Hurst alipofanya hivyo mwaka 1966.
Kama hiyo haitoshi, Mbappe ni mchezaji wa pili (baada ya Vava) kufunga bao katika mechi za fainali kwa misimu miwili mfululizo ya Kombe la Dunia (2018 na 2022).
Pia, Mbappe ndiye mfungaji bora wa mechi za fainali za Kombe la Dunia. Mshambuliaji huyo ana mabao manne.
Published:


