MADRID, Hispania
JINA la mpachikaji mabao wa Levante, Etta Eyong, si tu linatakisa La Liga, bali pia limeingia kwenye rada za klabu kubwa za Ligi Kuu ya England (EPL).
Arsenal, Manchester United, Chelsea na West Ham United ni miongoni mwa klabu zinazohaha kuinasa saini ya mshambuliaji wa kati huyo wa kimataifa wa Cameroon.
Kwa msimu huu wa La Liga, Eyong mwenye umri wa miaka 22, ameitikisa La Liga kwa uwezo wake wa kufunga mabao, ambapo ameshapachika mara sita na kutoa ‘asisti’ tatu.
Akiwa amehusika katika mabao tisa, Eyong amezidiwa na Kylian Mbappe pekee, ambaye amechangia mabao 15 katika kikosi cha Real Madrid msimu huu, akifunga 13 na kutoa asisti mbili.
Baba staa wa tenesi
Endapo angefuata nyayo za baba yake, Joseph, basi leo hii Eyong angekuwa mchezaji wa tenesi na si soka. Mzee wake huyo alikuwa staa wa tenesi huo Cameron.
“Baba yangu alinifundisha tenesi tangu nikiwa mdogo. Sikuwa mchezaji mbaya (wa tenesi) lakini niliacha baada ya kupoteza fainali, nikaamua kugeukia mchezo wa soka,” anasema.
Hata hivyo, hakuwa mtu pekee kwenye familia. Shangazi yake, Manuella Bekombo, alikuwa mshambuliaji wa timu ya soka ya taifa ya Cameroon.
“Ilikuwa ngumu kufika hapa nilipo kwa sababu hatukuwa na fedha, nililazimika kutembea hadi kilometa 10 kufuata mazoezi,” amesema Eyong.
Kutoka Cameroon hadi Hispania
Januari, 2022, maskauti wa klabu ya Cadiz walimnasa na kumpeleka katika ‘academy’, ambapo alimaliza msimu uliofuata (2023-24) akiwa amefunga mabao 14.
Ni kutokana na uwezo wake huo, Eyong alisajiliwa na Villarreal, ambapo alijiunga na timu ya vijana iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja Tatu. Alifunga mabao 19.
Kuziba pengo la Lewandowski
Kwa upande mwingine, Barcelona nayo imeripotiwa kuitolea macho saini yake, ikiamini anafaa kuziba pengo la Robert Lewandowski anayeelekea ukingoni mwa maisha yake ya soka.
Huku ikielezwa kuwa Lewandowski ataondoka Barcelona mwishoni mwa msimu huu, zipo picha zinazomuonesha Eyong akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo alipokuwa na umri wa miaka 17.
“Nilipokuwa mdogo, nilikuwa nikitazama mechi za (Samuel) Eto’o akiwa Barcelona,” amesema Eyong, pia akimtaja staa mwingine wa zamani wa Barcelona, Lionel Messi, kuwa ni mchezaji bora zaidi katika ulimwengu wa soka.
Kutua England Januari?
Eyong, ambaye wachambuzi wa La Liga wanamfananisha na Erling Haaland, alijiunga na Levante miezi miwili iliyopita akitokea Villarreal, usajili wake ukigharimu euro milioni tatu tu.
Ni kwa maana hiyo, nyota huyo hatoweza kuondoka Levante ifikapo Januari, mwakani, kwani sheria haziruhusu mchezaji kutumikia klabu tatu tofauti katika msimu mmoja.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Levante, Jose Danvila, amezungumzia uwezekano wa klabu hiyo kumuuza Eyong ifikapo mwishoni mwa msimu huu wa 2025-26.
“Hatujapokea ofa yoyote kutoka Ligi Kuu ya England. Tulipokea ofa moja (nje ya England) lakini tumeikataa. Nimesoma stori nyingi kuhusu Etta na ni kweli anawaniwa, lakini hatauzwa Januari,” amesema.
Published:


