25.9 C
New York

Ramaphosa amjibu Trump ‘kususia’ Mkutano G20

Published:

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemkosoa mwenzake wa Marekani, Donald Trump, kwa hatua yake ya kugoma kuhudhuria Mkutano Mkuu wa G20 utakaofanyika Johannesburg baadaye mwezi huu.

Awali, Trump aliweka wazi kuwa hakuna kiongozi wa Marekani atakayekanyaga kwenye Mkutano huo unaokutanisha mataifa 20 yenye maendeleo makubwa kiuchumi duniani.

Kwa miezi kadhaa sasa, Trump na Serikali ya Marekani kwa ujumla wamekuwa wakiishutumu Afrika Kusini kwa madai ya kuwatesa, ikiwamo kuwaua, watu wenye ngozi nyeupe nchini humo.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amesema kitendo cha Marekani kususia Mkutano wa G20 ni hasara kwao na si kwa Afrika Kusini.

Mkutano wa G20 unatarajiwa kuanza kati ya Novemba 22-23, mwaka huu, lakini Trump amesema ni aibu kwa Afrika Kusini kuwa mwenyeji.

Hivi karibuni, alisema Afrika Kusini haipaswi kuwa sehemu ya G20 kutokana na kile alichokiita kuwa ni udhalimu dhidi ya watu weupe wanaoishi nchini humo.

“Hakuna kiongozi wa Marekani atakayehudhuria kwa kuwa bado vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinaendelea (Afrika Kusini),” amesema Trump.

Related articles

Recent articles