KYIV, Ukraine
MAWAZIRI wawili wa Serikali ya Ukraine wametangaza kujiuzulu baada ya kashfa ya rushwa kuitikisa sekta ya nishati nchini humo. Waliotangaza kuachia ngazi ni Waziri wa Nishati, Svitlana Grynchuk, na mwenzake wa Sheria, Herman Halushchenko, likiwa ni agizo la Rais Volodymyr Zelensky.
Hatua ya Rais Zelensky kuagiza wajiuzulu ilikuja baada ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa kuibua ‘upigaji’ wa Dola za Marekani milioni 100 kwenye sekta ya nishati.
Kile kilichoelezwa na Taasisi hiyo ni kwamba Waziri Halushchenko na baadhi ya vigogo wa Serikali walihujumu miradi ya kukarabati miundombinu ya nishati iliyoharibiwa na mashambulizi ya Urusi.
Mbaya zaidi, miongoni mwa waliotajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha za umma ni watu wa karibu wa Rais Zelensky. Miongoni mwao, limo jina la aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, Oleksiy Chernyshov, na mfanyabiashara maarufu, Timur Mindich.


