Na mwandishi wetu, Gazetini
SIASA za Afrika Kusini zimefungua ukurasa mpya baada ya binti wa Rais wa zamani wa Taifa hilo, Jacob Zuma, kushitakiwa kwa tuhuma za ugaidi.
Wengi wameshangazwa kusikia kuwa mashitaka yanayomkabili Duduzile Zuma-Sambudla mwenye umri wa miaka 43 yanatokana na kile alichokifanya miaka minne iliyopita.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka, mwanasiasa huyo wa upinzani alitumia mtandao ya kijamii kuhamasisha maandamano yaliyosababisha machafuko makubwa nchini humo.
Haijasahaulika kuwa maandamano hayo yalikuja baada ya Rais Zuma, ambaye aliiongoza Afrika Kusini kwa miaka tisa, kuhukumiwa kifungo cha gerezani mwaka 2021.
Itakumbukwa, machafuko hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea Afrika Kusini tangu ilipopata uhuru mwaka 1994, yalishika kasi katika majimbo ya KwaZulu-Natal na Gauteng na kusababisha vifo vya watu 300 na uharibifu wa mali zenye thamani ya Dola bilioni 2.8.
Kwa sasa, Zuma-Sambudla ni mbunge wa Chama cha upinzani cha uMkhonto weSizwe (MK) kinachoongozwa na baba yake aliyeondoka Chama tawala, African National Congress (ANC), tangu alipoachiwa huru kwa shinikizo la maandamano ya raia.
Kile kinachoelezwa na waendesha mashitaka ni kwamba Zuma-Sambudla alitumia ushawishi wake kuhamasisha vurugu kupitia kurasa zake za mtandao ya kijamii.
Waendesha mashitaka wanatumia baadhi ya ‘post’ zake za wakati huo wa machafuko ya mwaka 2021, ukiwamo alioandika:
“Fanyeni uharibifu wa barabara, viwanda, maduka na majengo ya serikali hadi pale rais mstaafu (Zuma) atakapoachiwa.”
Hata hivyo, kwa upande wake, Zuma-Sambudla amekana mashitaka, pia wawili anayemsimamia akiziita hoja za Serikali kuwa ni dhaifu.
Zuma-Sambudla ni nani? Alizaliwa na kukulia Msumbiji, ambako baba yake alikimbilia baada ya miaka 10 ya kutumikia kifungo cha gerezani nchini Afrika Kusini.
Huyo ni miongoni mwa watoto watano wa Zuma aliowapata katika ndoa yake na Kate Mantsho aliyejitoa uhai mwaka 2000. Zipo taarifa zingine zikidai kuwa Zuma ana watoto 20 katika mahusiano yake na wanawake mbalimbali.
Wakati fulani, hasa miaka ya 2010, kaka yake aitwaye Duduzane ndiye aliyekuwa na jina kubwa katika siasa za Afrika Kusini, ambapo alikuwa akihusishwa na familia ya Gupta inayoeleweka kwa kashfa za rushwa nchini humo.
Kwa upande wake, licha ya kuolewa na mfanyabiashara tajiri Lonwabo Sambudla na kufunga ndoa ya kifahari mwaka 2011, Zuma-Sambudla alijiweka mbali na vyombo vya habari. Alikuwa ni mama wa nyumbani tu, wakati huo akiwa na watoto wawili.
Ni baada ya kuachana na mumewe mwaka 2017, ndipo alipoanza kujisogeza kwenye siasa, akionekana mara kwa mara akiwa na baba yake katika matukio mbalimbali.
Hata baada ya Zuma kuondoka Chama tawala, ANC, na kujiunga na MK, Zuma-Sambudla hakubaki nyuma. Alimfuata na hatimaye kupata nafasi ya ubunge wa upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Pia, akateuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Umoja wa Afrika.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wachambuzi wa siasa barani Afrika, akiwamo Prof. Bheki Mngomezulu, wanaamini mashitaka yanayomkabili ni matokeo ya uadui uliopo kati ya baba yake na Serikali ya Chama tawala, ANC.
“Ni siasa tu. Kama si kuwa binti wa Rais wa zamani, huenda haya mashitaka yangeshatupiliwa mbali,” anasema Prof. Mngomezulu.
Published:


