23.5 C
New York

Afrika na safari ya Kombe la Dunia 2026 (1) – Tunisia

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Tunisia. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Tunisia ‘Carthage Eagles’ ilikata tiketi ikiwa na matokeo mazuri yaliyoiwezesha kukaa kileleni mwa Kundi H. Ni baada ya ushindi wa mechi tisa kati ya 10 za kufuzu. Ilikusanya pointi 28, ilifunga mabao 22 na haikuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Safari yao ya mechi za kufuzu chini ya kocha Jalel Kadri, ambaye alikuwa na kikosi hicho Kombe la Dunia mwaka 2022, ilianza kwa ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya Sao Tome na Malawi.
Hata hivyo, Kadri alifukuzwa baada ya kufanya vibaya katika michuano ya AFCON ya mwaka 2024, hivyo kocha wa muda, Montassar Louhichi, akaiongoza Tunisia kushinda mechi dhidi ya Guinea ya Ikweta na kupata suluhu mbele ya Namibia.
Kocha mkongwe, Faouzi Benzarti, aliajiriwa lakini alifukuzwa baada ya miezi miwili tu, akiponzwa na mfululizo wa matokeo mabaya.
Nyota wa zamani wa Tunisia, Kais Yaakoubi, alikabidhiwa benchi la ufundi kwa miezi kadhaa, kabla ya kuondoshwa na kumpisha Sami Trabelsi aliyeajiriwa mwanzoni mwa mwaka huu.
Trabelsi aliikuta timu ikiwa tayari iko kileleni mwa msimamo wa Kundi H na kuiongoza kushinda mechi sita mfululizo zilizoiwezesha kujihakikishia nafasi ya kwenda Kombe la Dunia ikiwa na mechi mbili mkononi.
Katika mechi sita za ushindi, mchezaji aliyekuwa na mchango mkubwa zaidi kwa kocha huyo ni staa wa Al Ahly, Mohamed Ben Romdhane, ambaye kwa wakati tofauti alifunga mabao manne, yote akitokea benchi.
Hii inakuwa mara ya saba kwa Tunisia kushiriki Kombe la Dunia. Ni mara ya tatu mfululizo kwa Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika kucheza michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hata hivyo, licha ya ushiriki wao wa mara kwa mara, Tunisia haijawahi kuvuka hatua ya makundi. “Kama tunataka kufika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia, tunapaswa kupambana na kujiandaa kwa mechi kubwa,” amesema kocha Trabelsi.
Katika fainali zilizopita za mwaka 2022 nchini Qatar, Tunisia iliwashangaza wengi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya vigogo wa soka la Ulaya, Ufaransa.
Historia ya Kombe la Dunia inaitambua Tunisia kuwa ilikuwa ndiyo timu ya kwanza ya Afrika kupata ushindi katika michuano hiyo ilipoifunga Mexico mabao 3-1 mwaka 1978.

Related articles

Recent articles