12.5 C
New York

Maria Corina Machado; ‘Mwanamke wa shoka’ aliyempindua Rais Trump

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
NI ukweli usiopingika kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ameumizwa na kitendo cha kutoitia mkononi tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu. Imemuuma mno!
Kuthibitisha hilo, Ikulu ya Marekani imewakosoa waandaaji wa tuzo hiyo ikisema haikutenda haki kumpuuza Rais Trump, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya migogoro mingi duniani, ukiwamo wa Israel na Palestina.
Na badala yake, waandaaji wa tuzo hiyo walimtangaza mwanamke maarufu katika siasa za nchini Venezuela, Maria Corina Machado ‘Iron Lady’ kuwa mshindi.
Kwa mujibu wa historia, Maria Corina anaibeba kwa mara ya kwanza na anakuwa mwanamke wa 20 kati ya washindi 143 tangu tuzo hizo zilipoanza mwaka 1901.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, zamani ukifahamika kwa jina la Twitter, Kamati ya Nobel ilimtangaza Maria Corina na kupongeza jitihada zake katika kupambania haki ya kidemokrasia kwa watu wa Venezuela.
Je, ni nani huyo Maria Corina, ambaye wengi wanamtaja kuwa ni ‘Mwanamke wa Shoka’? Kwa ufupi, ni kiongozi wa upinzani nchini Venezuela na mwaka jana alizuiwa kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu.
Maria Corina, kiongozi wa Chama cha Vente Venezuela mwenye umri wa miaka 58, amekuwa akiikosoa Serikali ya Venezuela, hasa ubinafsishaji wa baadhi ya kampuni, ikiwamo ile ya mafuta ya PDVSA.
Wakati huo huo, ushawishi wake mkubwa kwa wananchi wa Venezuela unatokana na shinikizo lake kwa Serikali akiitaka kuwa na programu za kuondosha umasikini.
Msomi huyo wa Shahada ya Uhandisi wa Viwanda na Shahada ya Uzamili ya Uhasibu, alizaliwa Oktoba 7, 1967, mjini Caracas, na ni wa kwanza katika familia yenye watoto wanne.
Maria Corina, ambaye ni mama wa watoto watatu, aliingia katika siasa mwaka 2002 baada ya kuanzisha taasisi ya kiraia ya Sumate iliyokuwa ikikosoa utawala wa Rais wa wakati huo, Hugo Chavez.
Hata baada ya Chavez kuondoka, Maria Corina ameendelea kuwa mkosoaji wa Serikali ya Rais wa sasa, Nicolas Maduro, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2014.
Mwaka jana, akiwa kwenye nafasi nzuri ya kuwania kiti cha urais dhidi ya Rais Maduro, Mahakama ilimpiga ‘stop’ kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa madai ya rushwa na kuunga mkono hatua ya Marekani kuiwekea vikwazo Venezuela.
Ikumbukwe, ni kutokana na hatua hiyo, Edmundo Gonzalez Urrutia alichukua nafasi yake na kuwania urais kwa upande wa upinzani.
Leo hii, viongozi wenzake wa upinzani, wakiwano washauri, wanashikiliwa na polisi kwa shutuma mbalimbali, wengine wakilazimika kukimbia nchi ili kuukwepa mkono mrefu wa Serikali ya Rais Maduro.
Mathalan, Gonzalez Urrutia aliyegombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, inaelezwa kuwa amehamishia maisha yake nchini Hispania.
Hata kwa upande wa Maria Corina, ambaye aliungana na jumuhiya za kimatafa kupinga ushindi wa Rais Maduro, amekuwa akiishi mafichoni akihofia kutiwa nguvuni.
Hajulikani alipo kwa sasa, ingawa taarifa rasmi zinaeleza kuwa Maria Corina hajaondoka nchini Venezuela. Kamati ya Nobel nayo ilithibitisha hilo.
“Kwa mwaka jana, Machado amelazimika kuishi mafichoni, licha ya vitisho dhidi ya maisha yake. Ameendelea kuishi nchini (Venezuela), uamuzi ambao umewavutia mamilioni ya watu,” ilieleza taarifa ya Kamati hiyo.
Licha ya kutojulikana aliko, bado Maria Corina ameendelea kuwa bega kwa bega na wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii.
Agosti, mwaka jana, alijitokeza na kuungana na wafuasi wake walioandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi huo wa Julai.
Aidha, tuzo ya Nobel ni mwendelezo wake wa kuzoa ushawishi kimataifa. Mwaka jana, Umoja wa Ulaya (EU) ulimpa tuzo ya haki za binadamu. Ni tuzo ambayo pia alikabidhiwa Gonzalez Urrutia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img