JONANNESBURG, Afrika Kusini
IJUMAA ya wiki hii, mabosi wa klabu ya Kaizer Chiefs walifikia makubaliano ya kutangaza kumfuta kazi Nasreddine Nabi.
Kocha huyo wa kimataifa wa Tunisia, amefukuzwa na ‘Amakhosi’ akiwa ameinoa timu hiyo kwa msimu mmoja tu. Kaizer walimtangaza Julai, mwaka jana, wakati huo Nabi akiwa ametoka kuachana na vigogo wa soka la Morocco, FAR Rabat.
Kwa msimu wake mmoja, licha ya Kaizer kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye msimao wa Ligi Kuu, mashabiki wa klabu hiyo watamkumbuka kwa ubingwa wa Nedbank Cup, taji la kwanza kwao ndani ya miaka 10 ya hivi karibuni.
Msimu huu, akiwa amekaa kwenye benchi katika mechi nne tu, mabosi waliamua kumfungashia virago. Ni baada ya kufungwa mechi tatu kati ya hizo.
Aidha, takwimu za jumla zinaonesha hivi; ameondoka akiwa ameliongoza benchi la ufundi katika mechi 35. Alishinda 12, sare tisa na kufungwa mara 14.
Katika mechi hizo 35, Kaizer iliweza kupachika mabao 39 lakini safu yake ya ulinzi haikuzuia nyavu zake kutikiswa mara 42.
Kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kufungiwa, Nabi alikosa mechi 11 za Kaizer, licha ya kwamba alikuwa ndiye kocha mkuu.
Wasaidizi wake, Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze, walishinda saba kati ya hizo 11 walizosimamia timu na kwa sasa wamepewa mikoba ya Nabi hadi mwishoni mwa msimu huu.
Published:


