WASHINGTON DC, Marekani
IKULU ya Marekani imeikosoa Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel ikisema haitendi haki katika kutangaza washindi. Kwa mujibu wake, tuzo ya mwaka huu ilipaswa kwenda kwa Rais Donald Trump na si aliyetangazwa, ambaye ni mwanaharakati wa siasa chini Venezuela, María Coria Machado.
Kabla ya mshindi kutangazwa hivi karibuni, Rais Trump alishaonesha kuitamani tuzo hiyo kutokana na jitihada zake za kusuluhisha migogoro duaniani. Mathalan, Rais Trump amekuwa na mchango mkubwa katika makubaliano ya kumaliza vita yaliyofikiwa kati ya Israel na wapiganaji wa Palestina, Hamas.
Akizungumzia Rais Trump kuikosa tuzo hiyo kupitia ukurasa wa ‘X’, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya Marekani, Steven Cheung, amesema:
“Kamati inaangalia zaidi siasa na si amani. Rais Trump ataendelea kushughulikia amani, kumaliza vita na kuokoa Maisha.”
Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani, akiwamo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamekuwa wakiamini kuwa Rais Trump anastahili tuzo hiyo ya Amani ya Nobel.
Historia inaonesha kuwa marais wanne wa Marekani wamewahi kuitwaa tuzo hiyo lakini ni Barack Obama pekee aliyeshinda akiwa madarakani.


