LONDON, Uingereza
NI wiki chache tu zimepita tangu msimu huu (2025-26) wa soka la Ulaya ulipoanza lakini tayari baadhi ya makocha wameonja ‘joto la jiwe’ kwa kupoteza ajira katika klabu zao.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya England (EPL), Nuno Espirito Santo amekuwa kocha wa kwanza kupoteza ajira baada ya Nottingham Forest kumfukuza Septemba 8, mwaka huu.
Mreno huyo ametimuliwa baada ya ugomvi wake na mmiliki wa klabu hiyo, Evangelos Marinakis, ambaye ameziba pengo lake kwa kumpa ajira kocha wa zamani wa Tottenham, Ange Postecoglou.
Hata hivyo, upepo mbaya wa kufukuzwa unaweza kuwakumba kocha wa West Ham United, Graham Potter, na mwenzake wa Manchester United, Ruben Amorim, endapo timu hizo zitaendelea kupata matokeo mabovu.
Msimu uliopita, makocha saba wa EPL walipoteza kazi, wakiwamo Erik ten Hag, Russell Martin, Julen Lopetegui, Sean Dyche na Postecoglou.
Kufikia hatua hii ya msimu, La Liga haijashuhudia kocha aliyefukuzwa, ingawa msimu uliopita ulimalizika kwa makocha sita kupoteza ajira.
Iko hivyo pia kwa Serie A. Hakuna kocha aliyetimuliwa. Msimu uliopita, makocha tisa walifutwa kazi, wakiwamo Daniele De Rossi, Ivan Juric, Paulo Fonseca, Thiago Motta na Claudio Ranieri.
Mambo ni moto Bundesliga, ambako Erik ten Hag amekuwa kocha wa kwanza kufukuzwa. Bayer Leverkusen ilimfuta kazi akiwa amekaa kwenye benchi kwa siku 62 tu. Ni baada ya kukosa ushindi katika mechi tatu za mwanzoni mwa msimu huu wa Bundesliga.
Msimu uliopita, Bundesliga ilishuhudia makocha sita wakipoteza kazi. Miongoni mwao ni Nuri Sahin, Marco Rose na Ralph Hasenhuttl.
Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) haina kocha aliyefungashiwa virago kufikia hatua hii ya msimu wa 2025-26. Msimu uliopita, makocha saba walifukuzwa.
Published:


