15.5 C
New York

Nigeria na janga la hali ya usalama

Published:

LAGOS, Nigeria
KATIKA baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria, raia wanalazimika kuwalipa fedha waasi ili tu waishi kwa amani. Hilo limeshuhudiwa katika Kijiji cha Sabon Birni na maeneo mengi ya Taifa hilo.
Mdororo huo wa hali ya usalama unaendelea, licha ya jitihada kubwa za Serikali kutafuta suluhisho la kuongezeka kwa vikundi vya waasi katika majimbo ya Kaskazini; Zamfara, Sokoto na Katsina.
Wakihojiwa na DW, kilio cha wakazi wa maeneo hayo ni ndugu zao kutekwa na kuuawa kila iitwayo leo. “Tunataka kuishi kwa amani,” anasema mkazi wa Sokoto, Suraju Mohammed.
Kutokana na ubabe wa vikundi hivyo, raia wamekuwa wakilazimika kulipa fedha ili kupewa nafasi ya kulima, ingawa baadaye huporwa mazao yao.
Hivi karibuni, waasi katika Jimbo la Sabongarin waliua watu 11 na kuteka wengine takribani 70, wakiwamo wanawake na watoto.
Jumuhiya za kimataifa zinaeleza kuwa kwa sasa baadhi ya maeneo nchini Nigeria hayako chini ya Serikali. Ni vikundi vya waasi ndivyo vinavyotawala.
Kwa wachambuzi wa siasa, kitendo hicho kinawafanya wananchi waanze kutokuiamini Serikali na kuamini haina nguvu mbele ya vikundi hivyo.
Katika hatua nyingine, Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya mazungumzo na vikundi vya waasi ili kurejesha hali ya usalama.
Lakini, baadhi ya wananchi wanaamini kufanya hivyo ni kuvipa nguvu vikundi hivyo. “Wameua watu wengi. Kwanini tukae nao kuomba amani? Wanapaswa kushitakiwa,” anasema Aisha Tukur, mkazi wa Jimbo la Zamfara.
Umaimah Abubakar, mkazi wa Kijiji cha Ranganda, ambaye amelazimika kuikimbia nyumba yake na kuhamia katika kambi ya watu wasio na makazi, anasema: “Endapo Serikali haitaongeza juhudi, waasi wataendelea kutusumbua tu.”
Lakini, wakati wengi wakidhani vikundi hivyo ni vya kisiasa pekee, vipo vinavyoshikilia baadhi ya maeneo na kulazimisha kutumika kwa sheria za Dini ya Uislam (Sharia).
Kwa pamoja, bila kuingiliana katika mipaka yao na wakati mwingine kushirikiana, vikundi vya kisiasa na vile vya dini vimewafanya wakazi wa eneo la Kaskazini mwa Nigeria kukosa amani, kushindwa kushiriki katika shughuli za kiuchumi, ikiwamo kilimo, na sasa wanakabiliwa na janga la njaa.
Kuthibitisha hilo, ripoti ya hivi karibuni ya Programu ya Chakula ya Umoja wa Mataifa (WFP) inaeleza kuwa wananchi wa Nigeria takribani milioni 31 wanakabiliwa na uhaba wa chakula.
Aidha, hali ni mbaya zaidi kwa watoto, ambapo zaidi ya milioni tano wana utapiamlo kutokana na ukosefu wa chakula, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN).

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img