Benki inayoongoza nchini Tanzania, NMB, imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika kipindi cha Nusu ya Kwanza ya mwaka 2021.
Faida baada ya kodi ya mapato imeongezeka kwa asilimia 43 na kufikia Shilingi bilioni 134, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 94 kipindi kilichoishia Juni 2020.
Aidha, ufanisi huu mkubwa umetokana na ongezeko la biashara na miamala, udhibiti wa gharama za uendeshaji, na ubora wa mikopo inayotolewa.
Mapato ya Benki yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia Shilingi bilioni 463 katika kipindi kilichomalizikia mwezi Juni 2021, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 387 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana.
Mapato haya yamechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za Serikali.
Vilevile, mapato yasiyotokana na riba yameongezeka kwa asilimia 17 hadi kufikia Shilingi bilioni 140, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 119 za kipindi kama hicho mwaka 2020.
Ongezeko la mapato yasiyo ya riba yalichangiwa na ongezeko la miamala ya kibenki kutokana na huduma nzuri zinazotolewa na benki, mahusiano mazuri na wateja, na uwekezaji katika mifumo ya kidigitali.
Kama hiyo haitoshi, Benki ya NMB imeendeleza ufanisi wa kiuendeshaji, sanjari na malengo makuu ya kimkakati pamoja na viwango elekezi vya ufanisi vilivyowekwa na msimamizi wa mabenki, yaani Benki Kuu ya Tanzania.
Katika kipindi hiki cha Nusu ya Kwanza ya mwaka 2021, uwiano wa matumizi yasiyo ya riba na mapato halisi umeimarika hadi asilimia 47, kutoka asilimia 56 katika kipindi kama hiki mwaka jana.
Uwiano huu wa asilimia 47 uko ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 55 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Benki itaendelea kutilia mkazo uimarishaji wa ufanisi, huku ikiboresha uwekezaji katika teknolojia na vipaumbele vya kimkakati ili kuendeleza utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Pia, katika kipindi hiki cha Nusu ya mwaka 2021, ubora wa mali za NMB uliimarika kutokana na mikakati thabiti ya kuimarisha mikopo ya benki. Katika kipindi hiki, uwiano wa mikopo uliimarika hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 6.9 katika kipindi kama hiki mwaka jana, ikiwa ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 5 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mizania yake ikiwa na ukuaji endelevu, hivyo kuonesha ilivyoweka misingi bora na imara ya uhusiano wake na wateja. Mikopo ilikuwa kwa asilimia 11 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.2 kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021, ukilinganisha na Shilingi trilioni 4 katika kipindi kama hiki mwaka jana.
Amana za wateja zilikua kwa asilimia 8 hadi kufikia Shilingi trilioni 5.8, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 5.5 katika kipindi kama hiki mwaka jana, hii ikionesha mazingira mazuri yaliyowekwa na Benki katika uhusiano wake na wateja.
Katika kipindi hiki, mali za Benki zimeongezeka kwa asilimia 6 hadi kufikia Shilingi trilioni 7.6, ukilinganisha na Shilingi trilioni 7.2 katika kipindi kama hiki mwaka jana.
Akizungumzia mafanikio haya makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema:
“Tunajivunia ufanisi bora na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya makubwa ya nusu ya mwaka 2021 ni kielelezo cha imani kubwa ya wananchi na wateja kwa benki yao ya NMB, ufanisi wa wafanyakazi wa benki ya NMB, utekelezaji bora na usimamizi mzuri wa mpango mkakati wa benki.”
Aliongeza: “Tunazidi kujikita katika misingi imara ambayo tumeshaijenga ikiwa ni pamoja na mizania bora ya benki, mtaji mkubwa, matawi mengi, uwezo mkubwa kidijitali, na wafanyakazi bora ili kuweza kusukuma mbele biashara yetu ya benki.
Tukiangalia mbele, tunahamasika tukiona fursa mbalimbali zilizo mbele yetu kutokana na kuzidi kuimarika kwa uchumi wa dunia, hasa baada ya madhara makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19, pamoja na hatua stahiki zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha sekta ya kibenki”.
Aidha, Ruth alimalizia kwa kusema NMB itaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wateja wake kwa ufanisi na kutoa huduma bora ili kuhakikisha benki hiyo inaendelea kuleta mafanikio kwa wawekezaji wake na pia kuwajibika katika jamii inayoizunguka.