RIYADH, Saudi Arabia
SERIKALI ya Saudi Arabia iko mstari wa mbele ikiiunga mkono Palestina katika harakati za za kutaka kutambulika kama nchi huru nje ya mikono ya Israel.
Katika jitihada zake, mwaka jana, Saudia ikishirikiana na Norway zilitangaza kampeni ya kutaka Palestina kupewa hadhi ya kuwa Taifa linalojiendesha bila kuingiliwa.
Hivi karibuni, Saudia na Ufaransa ziliratibu Mkutano, ambapo ajenda kuu ilikuwa ni namna ya kupigania Palestina katika harakati za kutambulika kama mamlaka kamili.
Hata hivyo, kwa kuwa Saudia haijazoeleka kupingana na mshirika wake wa miaka mingi, Israel, wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati wamezitafsiri kwa namna tofauti jitihada hizo.
Wakati wengine wakisema Saudia inafanya hivyo kutokana na sababu za kiutu, kwamba haifurahishwi na mateso wanayopitia Wapalestina kule Gaza, wapo wanaoamini kuwa hatua yao hiyo inatokana na masilahi binafsi.
Ndiyo, kwa mtazamo wa wachambuzi, Saudia kujitosa kuitetea Palestina ni katika ‘kujisafisha’ baada ya miaka mingi ya kukosolewa vikali na mataifa mengine ya Kiarabu.
Awali, kutokana na ukaribu wake na Israel ambao umedumu kwa miaka mingi, mataifa ya Kiarabu yaliitafsiri Saudia kuwa ni ‘msaliti’ dhidi ya Uislam.
“Wengi wanadhani uhusiano mzuri kati ya Saudi Arabia na Israel ulianza hivi karibuni. Ni ukaribu ambao umekuwepo tangu miaka ya 1960,” anasema Aziz Alghashian, mchambuzi wa siasa wa Saudia mwenye makazi yake mjini Washington, Marekani.
Hivyo, hatua yake ya sasa ya kusimama kidete ikitaka Palestina kupewa mamlaka kamili kama nchi, ni jitihada za kuondosha doa hilo mbele ya mataifa ya Kiarabu na jamii ya Uislam kwa ujumla.
Lakini pia, wakati huo ukiwa ni mtazamo wa baadhi ya wachambuzi, wapo wanaoenda mbali zaidi na kuzitaja sababu za kiuchumi kuchangia Saudia kujitosa kuitetea Palestina.
Msingi wa hoja ya wachambuzi hao ni kwamba Saudia imechoshwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, ikiamini vina mchango mkubwa katika kuathiri uchumi wake.
Mathalan, mamlaka za Saudia zinaona kutokuwapo kwa usalama katika eneo hilo kunazorotesha kwa kiasi fulani kasi ya maendeleo ya miradi yake mikubwa, ikiwamo ya mafuta, utalii na hata burundani.
Swali la kujiuliza; je, Saudia itafanikiwa katika mpango wake huo? Uingereza na Canada zimetangaza kuiunga mkono, zikitaka Palestina kuwa nchi huru.
Published:


