22.6 C
New York

TANESCO yatakiwa kubuni vyanzo vipya vya umeme

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea na kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya umeme.

Dk. Biteko amezungumza hayo leo Juni 4, 2025 kufuatia tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati ambayo imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa wizara/taasisi umeimarika kwa zaidi ya asilimia 95.


Pia amemtaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kupeleka umeme vijijini na kuwezesha vijiji vyote kupata umeme pia kuendelea na kasi ya kupeleka umeme vitongojini.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dk. Biteko amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara hususan, REA, TPDC na TANESCO kuunganisha nguvu katika kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ili ikue na kufanikiwa na hivyo kutimiza lengo la Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye matumizi ya nishati safi.

Dk. Biteko amekipongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati  kwa kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi na kukumbusha Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake  kuwa, zoezi hilo la tathmini linapaswa kuwa  ni endelevu kutokana na umuhimu wake katika kuboresha utendaji kazi.

“Sekta hii ni muhimu sana nchini kwa kuwa ni Sekta ya huduma na sekta ya uchumi hivyo ikilegalega italeta malalamiko, ningependa kuona sekta hii inaendelea kuwa na matokeo mazuri kwa wananchi.” amesema Dk. Biteko.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img