Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuwanusuru wazee kutoka kwenye umasikini kwa kuanza kuwalipa posho kila mwezi endapo hali ya uchumi itaruhusu.
Hayo yameelezwa leo Aprili 29,2025 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Christina Mnzava aliyetaka kufahamu mpango wa serikali kuja na sera ya kuwapatia posho wazee wote nchini kama inavyofanyika visiwani zanzibar.
“Ni kweli kwa upande wa Tanzania Visiwani wameanza utaratibu huo na sisi kwa sera yetu hii, ambayo ni ya mwaka 2003 moja ya maeneo ambayo yamewekewa mkazo ni pamoja na hili la kuangalia hali za kiuchumi na kuwanusuru wazee katika lindi la umasikini na changamoto za kiuchumi.Kwa hiyo nimelipokea na tutaendelea kulifanyia kazi kupitia ofisi ya Waziri Mkuu na wizara husika kuona kama hali itaruhusu hilo litatekelezwa,” amefafanua naibu waziri.


