PARIS, Ufaransa
KATIKA tasnia ya michezo, Teddy Riner ni staa wa judo aliyetwaa mara tano ubingwa wa michuano ya Olimpiki, lakini sasa ni mwanasiasa anayewania nafasi ya urais nchini Ufaransa, huku Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika Aprili, 2027.
Riner mwenye umri wa miaka 37, mbali na mataji matano ya Olimpiki, pia ni mshindi mara 11 wa ubingwa wa dunia katika mchezo wa judo.
Aidha, anagombea urais si tu akiwa hana uzoefu katika siasa, bali pia hana chama anachokiwakilisha. Anasimama akiwa mgombea binafsi.
Amekuwa akitumia kaulimbiu yake ya ‘La France qu’on aime’ (Ufatransa Tuipendayo), ambayo kwa sasa imejizolea umaarufu wa kutosha kwenye mitandao ya kijamii.
Wakati anatangaza nia ya kugombea urais kupitia ukurasa wake wa Instagram, watu zaidi ya milioni 28 walifuatilia.
Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa siasa za Ufaransa, mgombea aliye kwenye nafasi nzuri ya kushinda ni aidha awe mwanasiasa wa mrengo wa kulia au ule wa upinzani, yaani mrengo wa kushoto.
Hivyo, kitendo cha Riner kutokuwa na upande, kwa baadhi ya wachambuzi, itampa nafasi finyu ya kutimiza ndoto ya kuwa rais.
Katika ahadi zake, Riner ameweka wazi kuwa yeye si wa kulia wala kushoto, na badala yake anataka kuondosha tofauti hizo, pamoja na kuwawekea fedha mfukoni wananchi wa Ufaransa.


