WASHINGTON DC, Marekani
MARAIS wa mataifa makubwa matatu ya Marekani, Urusi na China wanatarajiwa kuwa na kikao chao kizito wiki ijayo mjini Beijing.
Wakati huo huo, vyanzo vingi vya habari vimeeleza kuwa Iran itajadiliwa katika meza ya viongozi hao lakini Ukraine inayozozana na Urusi haitogusiwa.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imethibitisha kuwa Rais wake, Donald Trump, atakaa mezani na Vladimir Putin wa Urusi na mwenzao wa China, Xi Jinping.
Tukio hilo la kihistoria litafanyika wakati Rais Trump atakapoingia China kuhudhuria Mkutano wa Asia-Pacific Economic Co-operation (Apec) katika Mji wa Shenzhen ulioko Kusini mwa China.
Rais Trump anatarajiwa kuingia Shenzhen usiku wa Jumatano, ambako atahudhuria kwa siku zote mbili za Mkutano huo utakaoshirikisha mataifa 21.
“Rais ameweka wazi, kwamba miongoni mwa hoja, atajadili kupungua kwa silaha za nyuklia duniani, ambazo Rais Trump anaamini uwepo wake ni hatari,” imeeleza taarifa ya Ikulu.


